Shirika la habari la Kipalestina, Shehab, liliripoti kuwa makundi ya walowezi yaliongeza mashambulizi yao dhidi ya eneo la msikiti wa Al-Aqsa, wakifanya vitendo vya uchokozi na kutekeleza ibada za Talmud katika viwanja vya msikiti huo, kinyume na hali ya utulivu iliyowekwa kihistoria.
Kulingana na Kituo cha Ma’ati cha Taarifa za Kipalestina, mwezi Oktoba 2025 uliona ongezeko kubwa la ukiukaji katika mji wa Al-Quds unaokaliwa kwa mabavu, ambapo matukio 408 yalirekodiwa yakihusisha majeshi ya Kizayuni na walowezi.
Miongoni mwa hayo, mashambulizi 25 dhidi ya msikiti wa Al-Aqsa yalithibitishwa, na jumla ya walowezi 18,963 waliingia katika eneo hilo takatifu.
Kituo hicho kilieleza kuwa wimbi la uvamizi lilifanyika sambamba na sikukuu za Kiyahudi, ambazo mara nyingi huambatana na mvutano mkubwa katika msikiti huo mtukufu wa Kiislamu.
Wapalestina 35 walijeruhiwa katika mashambulizi ya walowezi na uvamizi wa kijeshi mwezi uliopita. Aidha, mamlaka ya Kizayuni ilitoa amri nne za kufukuzwa, ikawakamata Wapalestina 33, na kutekeleza mashambulizi 94 tofauti.
Ripoti hiyo pia ilibaini mashambulizi 30 yanayohusiana na upanuzi wa makazi ya walowezi, kesi 21 za kubomoa nyumba na mali, na matukio 17 ya kunyang’anywa mali za Wapalestina.
Majeshi ya Kizayuni pia yaliweka vizuizi 65 na vituo vya ukaguzi, kuvamia nyumba 42, na kutekeleza matukio 40 ya kurusha risasi, ikiwemo mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.
Msikiti wa Al-Aqsa umeendelea kuwa kitovu cha mvutano, ambapo uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi chini ya ulinzi wa polisi huibua mapigano na kulaaniwa kimataifa.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Wadi Araba wa mwaka 1994 kati ya Jordan na Israel, Jordan inaendelea kuwa mlezi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika mji wa Al-Quds.
Jukumu hili lilithibitishwa tena katika makubaliano ya mwaka 2013 kati ya Mfalme Abdullah II wa Jordan na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, ambapo msikiti wa Al-Aqsa uliwekwa chini ya usimamizi wa Waqfu ya Kiislamu ya Jerusalem, inayosimamiwa na Wizara ya Awqaf, Mambo ya Kiislamu na Maeneo Matakatifu ya Jordan.
Ingawa kihistoria wageni wa Kiyahudi waliruhusiwa kutembelea eneo hilo kwa idhini ya Waqfu, sera za upande mmoja za Israel zimeendelea kudhoofisha mamlaka ya Waqfu hiyo.
Licha ya madai ya Israel kuwa hali ya utulivu wa kihistoria, ambayo inaruhusu Waislamu pekee kuabudu katika Al-Aqsa huku wengine wakitembelea, inaendelea kuheshimiwa, ushahidi wa video mara kwa mara umeonyesha walowezi wa Kiyahudi wakifanya sala na ibada za kidini chini ya ulinzi wa polisi wakati wa ziara zao.
Wapalestina kwa muda mrefu wameonya kuhusu sera za utawala wa Kizayuni za kuufanya msikiti huo kuwa wa Kiyahudi-Kizayuni, huku baadhi ya makundi ya Kiyahudi yenye misimamo mikali yakitoa wito wa kubomoa msikiti huo na kujenga hekalu la Kiyahudi mahala pake.
3495325