IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jihadi ya wajasiriamali Wairani imeifanya Marekani ikiri kushindwa katika vita vya kiuchumi

21:32 - January 30, 2022
Habari ID: 3474870
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jihadi ya wajasiriamali na wafanyakazi wa viwandani katika ngome ya uzalishaji imeifanya Marekani ikiri kuwa imeshindwa katika vita vyake vya kiuchumi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na idadi kadhaa ya wazalishaji na wadau wa sekta ya viwanda na akaongeza kuwa, kuna faida kwa wadau wenyewe wa sekta ya uchumi kuwataarifu wananchi kuhusu mafanikio waliyopata katika kukabiliana na vita vya kinafsi vya adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, mipango ya adui ya kuisambaratisha ngome ya uzalishaji imegonga mwamba; na akabainisha kwamba, katika hujuma hiyo dhidi ya uchumi wa nchi, maisha ya watu yalikumbwa na matatizo mbalimbali, lakini uzalishaji haukupigishwa magoti; na siku chache nyuma msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alitangaza kinagaubaga kuwa sera ya mashinikizo ya juu kabisa imepelekea Marekani kushindwa kiudhalili.

Ayatullah Khamenei ameutaja uzalishaji kuwa ni Jihadi na akaongeza kuwa, kusimama imara wazalishaji katika kukabiliana na hujuma dhidi ya uchumi na njama za adui za kuzuia uuzaji mafuta na gesi, kukata vyanzo vya fedha za kigeni na kuandaa mikakati ya kuzuia mabadilishano ya Iran na ulimwengu wa nje, ni jihadi na moja ya ibada kubwa kabisa.

Halikadhalika amesema: "kusambaratika kwa uchumi, kwa walivyodhani wenyewe ndani ya miezi michache, kungeandaa mazingira ya kuthibiti malengo yao maovu ya kisiasa, lakini alhamdulillah baada ya miaka kumi, ngome ya uzalishaji na uchumi nchini ingali iko imara."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo pia kuendeshwa kitaaluma sekta kubwa za viwanda na akasema, katika suala hili, inapasa kutumia ujuzi na uwezo wa vijana wenye vipawa, kama ambavyo kila mahali walipoaminiwa na kutakiwa wafanye kazi, vijana hao wameweza kung'aa kikwelikweli, kuanzia kwenye chanjo ya corona mpaka kwenye uundaji makombora yenye shabaha kali.

Kabla ya hotuba ya Ayatullah Khamenei, wadau 14 wa sekta mbalimbali za uzalishaji walipata fursa ya kutoa maoni na kueleza mitazamo yao.

4032336

captcha