IQNA

Raisi katika ujumbe wa Nowruz: Karne mpya ni ya watu wa Iran kuwa na nafasi na machango muhimu zaidi

10:13 - March 21, 2022
Habari ID: 3475063
TEHRAN (IQNA)- Katika ujumbe wake wa Nowruz au Nairuzi na mwaka mpya wa 1401 Hijria Shamsia, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja karne ya kumi na tano Hijria Shamsia kuwa ni karne ya Iran ya Kiislamu na zama za watu wa Iran kuwa na nafasi na machango muhimu zaidi.

Akizungumza kwa njia ya moja kwa moja akiwa katika Msikiti wa Jamia wa Khorsamshahr kusini magharibi mwa Iran Jumapili jioni, Sayyid Ebrahim Raisi amelipongeza taifa kwa kuanza mwaka mpya wa 1401 Hijria Shamsia na kuitaja karne ya kumi na tano kuwa ni karne ya Iran ya Kiislamu. Amesema: "Katika miaka minane ya vita vya kulazimishwa (vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Iran) Mashariki na Magharibi ya dunia zilisimama katika safu moja dhidi ya harakati ya kutaka kujitawala ya Iran, lakini hii leo wanashindana wao kwa wao kwa ajili ya kushirikiana na Iran; huu ndio ukubwa wa taifa la Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Sambamba na mazungumzo ya nyuklia huko Vienna, tumejitahidi kadiri tuwezavyo kukabiliana na vikwazo hivyo vya kidhalimu, huku tukitumia nyenzo za kisiasa na kisheria ili kukomesha jinai hiyo ya vikwazo.

Rais Ebrahim Raisi ameashiria kuwa, serikali ya Iran imezidisha biashara na majirani zake kwa manufaa ya wananchi na kuongeza kuwa: "Kumekuwepo ishara za ukuaji wa uchumi, uthabiti, ongezeko kubwa la thamani ya biashara ya nje ya Iran na mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta katika kipindi hiki."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali imerejesha mlingano katika siasa za nje kupitia diplomasia amilifu na kusema: Mafanikio makubwa zaidi ya nchi katika miaka ya karibuni ni kushindwa kwa fedheha sera ya mashinikizo ya juu kabisa ya Wamarekani, ambako kumefanikishwa na muqawama wa taifa la Iran. 

Mwishoni, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza matumaini yake kuwa mwaka mpya wa Hijria Shamsia utakuwa mwisho wa corona kote duniani, kumalizika vita na kukoma ukimbizi wa wanadamu katika nchi zote za dunia.

Ni vyema kutaja hapa kuwa, mwanzo wa miaka miwili ya Hijria Qamaria na Hijria Shamsia ni mmoja yaani hijra na tukio la kuhama Mtume Muhammad (saw) kutoka Makka na kwenda Madina katika mwaka wa 13 baada ya kupewa utume (mwaka 622 Miladia), lakini mwaka wa Qamaria unahesabiwa kwa kuzunguka mwezi mara 12 kandokando ya sayari ya dunia, na mwaka wa Shamsia unahesabiwa kwa dunia kuzunguka jua mara moja. Kwa kuwa mwaka wa Hijria Shamsia una siku 365, kila mwaka huwa na siku 11 zaidi ya mwaka wa Hijria Qamaria ambao huwa na siku 354.

135316

Kishikizo: raisi iran nowruz
captcha