IQNA

Mwaka mpya wa Hijria Shamsia

17:43 - March 18, 2016
Habari ID: 3470204
Tarehe 20 au 21 Machi husadifiana na tarehe Mosi Farvardin, siku ya kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia, siku ambayo ni maarufu kama Nowruz au kwa Kiswahili Nairuzi. Kuwadia kwa mwaka mpya wa Hijria Shamsia ambao aghalabu huadhimishwa Iran huenda sambamba na kuingia msimu wa machipuo na mabadiliko katika miti, mimea maua na majani.

Machipuo hayo hujiri katika nchi za kaskakzini mwa ikweta. Katika kipindi hicho, jua huwa katikati mwa ikweta.Kwa hakika mabadiliko hayo, huashiria kumalizika msimu wa baridi na kuwadia kipindi cha upepo mwanana wenye kuleta utulivu wa moyo. Katika msimu huu mimea huonekana ikiwa imechangamka na kunawiri huku ikiashiria kuwa na nishati na uchangamfu wa hali ya juu ikilinganishwa na vipindi vingine vya misimu ya mwaka. Kwa kifupi mandhari huwa ni ya kijani kibichi hali inayoashiria kuweko uhai. Bustani hunawiri kwa maua yaliyochanua na kunawiri kwa rangi tofauti tofauti. Watu ambao ni wa Mungu na wenye kushikamana na Allah na mafundisho yake, hupata ibra na mazingitio makubwa kupitia mabadiliko haya ya kuchipua mimea katika kuanza msimu huo wa machipuo kwa ajili ya kuleta mabadiliko ndani ya nafsi zao. Watu ambao ni wa Mwenyezi Mungu huzitumia lahadha za kuingia mwaka mpya na Sikukuu ya Nairuizi kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu alete mabadiliko katika nafsi zao na vile vile humuomba Mwenyezi Mungu abadilishe hali zao na kuwa bora ya hali. Watu hawa humuomba Allah alete hali ya nishati na machipuo yaani mabadiliko katika nyoyo zao. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitizia juu ya ulazima wa kuweko mabadiliko ya ndani ya mwanaadamu katika kila mwaka na kusema, mabadiliko ya kila mwaka ya kalenda ya Hijria Shamsia ambayo yanasadifiana na mabadiliko katika ulimwengu wa mimea, majani, maua na miti, ni fursa ambayo mwanaadamu anapaswa kuitumia ili alete mabadiliko ya kiroho, kimaanawi, kifikra na kimaada na dua ambayo husomwa katika lahadha za kuingia mwaka mpya ni somo la mabadiliko haya. Katika dua hii tunamuomba Mwenyezi Mungu alete mabadiliko katika hali zetu na kuzifanya kuwa hali bora kabisa." Dua hiyo inasema:

یا مقلّب القلوب والابصار،

یا مدبّر اللّیل والنّهار،

یا محوّل الحول والاحوال،

حوّل حالنا الی احسن الحال

Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana! Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.

Mwanzoni kabisa mwa dua hii tunaanza kwa kusema:

یا مقلّب القلوب,

Yaani Ewe Mgeuzaji wa nyoyo!. Ukweli wa mambo ni kuwa, moyo ni kitovu cha mielekeo na huba na vile vile ni kituo cha mapenzi na chuki. Kiungo hiki muhimu kimepewa jina la قلب yenye maana moyo kutokana na kuwa daima kiungo hiki hukabiliwa na hali ya kubadilika na kugeuka. Kuna wakati moyo hujaa mapenzi, huba na huruma na kuwa sababu muhimu ya mvuto. Wakati mwingine moyo hujawa na hali ya chuki na kuwa sababu kukimbiwa. Kwa hakika mambo haya ni masuala muhimu tunayokumbana nayo katika maisha yetu ya kila siku. Kwa msingi huo basi, moja ya sababu za kugeuka na kubadilika mwanaadamu ni moyo na sababu ya moyo kubadilika na kugeuka ni Mwenyezi Mungu SWT. Kwa hakika yeye anaweza kubadilisha mapenzi na mapendano na kuwa chuki; na kubadilika chuki na adawa na kuwa huba na mapenzi.

Sehemu nyingine ambayo ni sababu ya mabadiliko na mageuzi katika maisha ya mwanadamu ni kuwa macho na kuwa na muono wa mbali. Tunasoma katika dua ya Nairuzi: Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Moja ya misingi muhimu ya kuleta mabadiliko ya ndani ni kubadilisha mitazamo na mielekeo. Kama mitazamo yetu itabadilika basi sisi pia hubadilika. Kwa hakika suala la tadbiri na kubadilisha usiku na mchana kunakofanywa na Mwenyezi Mungu ambapo kumekuja pia katika dua ya Nairuzi ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo kuyazingatia kwake hupelekea kumtambua Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 10 ya Surat An-Nabaa kwamba: Na tukaufanya usiku ni nguo.

Kwa mujibu wa maumbile ambayo Mwenyezi Mungu ameyaweka, pindi linapoingia giza na usiku, mwanadamu humili katika hali ya kulala na kupumzika katika wakati huo, kutokana na mchoko uliotokana na pirika pirika za kazi za kutwa nzima na hilo ni jambo la lazima ili aweze kurejesha tena nguvu zilizopotea kutokana na machovu. Na kwa muktadha huo aweze kuamka kesho na kuendelea na harakati za kutafuta riziki. Hivyo basi kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu wakati wa usiku ni fursa ya mtu kupumzika kutokana na harakati za kutwa nzima za kutafuta maisha na wakati wa mchana ni muda wa kutafuta maisha kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

"Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha”.

Wapenzi wasikilizaji usiku na mchana zinahesabiwa kuwa ni nguzo mbili muhimu za kuendelea uhai katika mgongo wa ardhi ambapo uwepo wa kila moja kati ya mawili haya ni jambo la dharura. Kwani kuishi katika nuru daima au katika kiza siku zote humfanya mwanadamu aangamie. Usiku na mchana kama yalivyo matukio mengine ni ishara mbili za uwepo wa Mwenyezi Mungu Mmoja anayeendesha mambo. Kwa hakika hapa duniani ni mahala pa mabadiliko na mabadiliko ya kimaada ni miongoni mwa mabadiliko yaliyoko duniani. Kwa kuzingatia uhakika huo, wanaadamu wanapaswa kupata ibra na mazingatio kupitia mabadiliko ya mimea na kuchipua majani na mandhari kuwa ya kijani kibichi na hivyo kuleta mabadiliko katika fikra zao, tabia zao na kadhalika.

Historia fupi ya Nairuzi

Nairuzi ni sherehe ambayo imedumu toka zama za kale na ingali inaadhimishwa. Kwa mujibu wa aghalabu ya ngano za kale na riwaya za kihistoria kuhusu Nairuzi, sikuu kuu hii ilianzishwa na mfalme Jamshid katika silisila ya tawala za Pishdadi. Jamshid alikuwa mfalme wa nne katika silisila ya watawala wa Pishdadi na anatambuliwa kama muasisi wa siku kuu ya Nairuzi. Jamshid alikuwa mfalme aliyependwa sana na wananchi. Inasimuliwa kuwa katika siku zake, nchi ilifika katika kilele cha utajiri wa mali. Ferdowsi malenga wa kihamasa Iran katika simulizi yake kuhusu kuibuka Nairuzi anasema wakati neema zilipokuwa nyingi katika nchi, aliwakusanya maafisa wote wa serikali na kuwashukuru. Jamshid aliwashukuru na kuwaenzi waliofanya kazi vizuri tarehe Mosi Farvardin ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Shamsia. Aliitaja siku hiyo kuwa ni siku ya Nairuzi yaani siku mpya na sherehe.
Pamoja na kuwa hakuna nyaraka kamili kuhusu historia ya Nairuzi, lakini hakuna shaka kuwa Nairuzi ni sherehe ya kale na ilikuwa katika ardhi ya Iran hata kabla ya kuwasili kaumu ya Arya. Kwa mujibu wa mtafiti Muirani Mehrdad Bahar, Nairuzi ni mila na desturi ya kale ambayo ilikuwepo millennia ya tatu kabla ya Miladia (Kuzaliwa Nabii Issa AS). Anaandika hivi: 'Sherehe hizo zilikuwa zikiadhimishwa na makabila ya asili ya wenye kuhamahama Iran.' Baadhi ya riwaya za kihistoria zinasema Nairuzi iliingia Iran mwaka 538 kabla ya Miladia baada ya Kourosh kuliteka eneo la Babol. Riwaya hizo zinasema kuwa katika kukaribisha Nairuzi, Kourosh wa Pili alikuwa na mpango maalumu wa kuboresha maisha ya askari wake, kusafisha na kudumisha unadhifu katika maeneo ya umma na nyumba binafsi sambamba na kuwaachilia huru wafungwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika maandishi yaliyokuwa kwenye majabali katika zama za Wakhamaneshi katika karne ya 6 kabla ya Miladia, watu wa zama hizo walikuwa wakifahamu vyema mila na desturi za Nairuzi. Wafalme wa silisila ya Wakhamaneshi walikuwa wakitekeleza marasimu maalumu za kuwadia Nairuzi katika eneo maalumu la ibada lililojulikana kama Takht-e Jamshid yaani Persepolis. Katika sherehe hizo maalumu wafalme walikuwa wakiwakaribisha watu kutoka kaumu na mataifa mbali mbali. Kila mwaka wawakilishi wa mataifa mbali mbali ya dunia, wakiwa wamevalia nguo zao za kikaumu na kitaifa walikuwa wakifika huko Takht-e Jamshid na kusherehekea siku kuu ya Nairuzi. Katika marasimu hiyo, walikuwa wakimletea mfalme wa Iran zawadi zenye thamani kubwa.
Nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, Mfalme Dariush wa Kwanza, katika mwaka wa 416 kabla ya Miladia alitengeneza sarafu za dhahabu kwa mnasaba wa Nairuzi. Sehemu moja ya sarafu hiyo ina taswira ya askari akirusha mshale. Katika zama za watalwa wa Washkani na Wassasani kuanzia karne ya 247 Kabla ya Miladia hadi karne ya 650 Miladia kuliendelea kufanyika sherehe za Nairuzi ambazo ziliadhimishwa kwa siku kadhaa mfululizo. Katika zama za Washkani siku kuu hii ilikuwa na duru mbili yaani Nairuzi ndogo na Nairuzi Kubwa. Katika zama za Wasassani, Nairuzi ilikuwa na duru ya Nairuzi ya Umma na Nairuzi Maalum. Nairuzi ya umma ilidumu kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe Mosi Farvardin na Nairuzi Maalumu ilikuwa siku ya sita ya Farvardin ambapo kulifanyika sherehe kubwa. Katika siku za tano za kwanza za Nairuzi kulikuwa na karamu kwa ajili ya umma ambapo pia wananchi walibainisha maombi yao. Katika siku ya sita ambayo ilikuwa ndio Nairuzi kubwa kulifanyika sherehe maalumu ya mfalme na watu wa karibu naye. Tunaweza kusema sherehe hiyo ilikuwa maalumu katika kasri la utawala.


Baada ya kuingia Uislamu katika ardhi ya Iran, Waislamu Wairani waliendelea kuadhimisha siku ya Nairuzi lakini kwa kuzingatia mafundisho, mila na desturi za Kiislamu. Katika zama za utawala wa Waseljuki walioanza kutawala Iran katika karne ya 10 Miladia kulifanyika mabadiliko katika kalenda kuhusu mwaka wa Shamsia. Jalaluddin Malik Shah Seljuki mnamo mwaka 467 Hijria Qamaria sawia na 1074 Miladia aliwataka wanahisabati na wataalamu wa falaki au elimu ya nyota akiwamo Omar Khayyam Nishaburi wachunguze namna ya kufanyia marekebisho kalenda iliyokuwepo wakati huo. Wataalamu hao walifikia natija kuwa siku ya kwanza ya Nairuzi isadifiane na siku ya kwanza ya msimu wa machipuo na ndio maana kalenda ya Iran ikapewa pia jina la 'Kalenda ya Jalali' au 'Maliki'. Kimsingi ni kuwa kalenda hii ilienda sambamba na kalenda ya kimaumbile kikamilifu. Kwa hivyo si tu kuwa Nairuzi iko katika siku ya awali ya machipuo, bali pia kalenda ya Jalali au Hijria Shamsia inaenda sambamba na misimu yote ya kimaumbile katika eneo hili la dunia. Mwaka wa kalenda ya Jalali hairudi nyuma hata siku moja na nukta hii ni kinyume cha Kalenda ya Miladia (Gregorian) ambayo baada ya kila miaka elfu 10 huwa na hitilafu ya takribani siku tatu.
Baada ya kudhihiri Uislamu Iran hasa katika zama za utawala wa silisila ya Wassafavi yaani karne za 10 na 11 Hijria Qamaria au 16 Miladia, sherehe za Nairuzi zilichanganywa na mila na desturi za Kiislamu na hivyo kupata uhai na ufahamu mpya. Hali kadhalika kuna riwaya za Kiislamu kuhusu umuhimu wa Siku Kuu ya Nairuzi jambo ambalo limefanya sherehe hizo zipate umuhimu miongoni mwa baadhi ya Waislamu . Imam Ja'afar Sadiq AS amenukuliwa akisema kuwa Nairuzi ni siku ya furaha na iliyobarikiwa. Kwa msingi huo Waislamu Wairani wanaitambua Nairuzi kama siku yenye furaha na baraka na wameiambatanisha na utamaduni wa Kiislamu-Kiirani.

Katika zama zetu hizi Nairuzi pia inazingatiwa na kuadhimishwa si tu nchini Iran bali katika maeneo mengi duniani hasa Asia, Ulaya na Afrika Mashariki. Mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO lilitangaza na kuisajili Nairuzi kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha Mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nairuzi. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nairuzi kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, siku kuu ya Nairuzi hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa wa urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali. Katika matini ya kuidhinishwa Nairuzi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeandikwa kuwa: "Sherehe za Nairuzi zina mizizi ya Kiirani ya zaidi ya miaka 3,000 na leo zaidi ya watu milioni 300 huadhimisha siku hii."
Leo Nairuzi inaadhimishwa kwa njia mbali mbali katika nchi ambazo katika zama za kale zilikuwa sehemu ya Iran au mataifa ambayo yameathiriwa na utamaduni na mila za Iran. Ingawa mataifa mengine yanasherehekea kwa njia tofauti lakini nukta ya pamoja ni kuwa sherehe hizo zimepewa jina la Nairuzi. Kati ya nchi ambazo Nairuzi husherehekewa ni kama vile Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kirghizstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Inafaa kuashiria hapa kuwa katika ustaarabu wa Kiswahili, Nairuzi huadhimishwa japo katika mwezi tofauti na ule wa mwanzo wa machipuo hapa Iran. Sherehe hizi hasa zinashuhudiwa Zanzibar ambapo Nairuzi hujulikana kama Nairuzi yaani siku ya mwaka au Mwaka Kogwa.

3482497

captcha