IQNA

Kiongozi Muadhamu asisitiza uzalishaji unaotegemea elimu na kutengeneza ajira katika mwaka mpya wa Hijria Shamsia

9:45 - March 21, 2022
Habari ID: 3475062
TEHRAN (IQNA)-Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1401 Hijria Shamsia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa kwa kuwadia sikukuu ya Nowruz au Nairuzina kuutaja mwaka mpya kuwa ni mwaka wa "uzalishaji unaotegemea elimu na kutengeneza ajira."

Ayatullah Ali Khamenei amelipongeza taifa kubwa la Iran na mataifa yote rafiki kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Nowruz na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imamu wa Zama, Hadhrat Baqiyatullah (AS) na kutoa mkono makhsusi wa kheri na baraka kwa familia za mashahidi, vilema wa vita na watumishi wa taifa katika nyanja mbalimbali za sayansi, afya, usalama na muqawama. Ameutaja mwaka mpya kuwa ni mwaka wa "uzalishaji unaotegemea elimu na kutengeneza ajira."

Ayatullah Khamenei ameutaja mwaka uliomalizika wa 1400 Hijria Shamsia kuwa uliandamana na heka heka na kusema: "Uchaguzi muhimu na mkubwa wa rais ulikuwa moja kati ya matukio muhimu ya mwaka uliopita ambako wananchi walishiriki katika uchaguzi huo licha ya hatari kubwa ya maambukizi ya corona na kuchagua serikali mpya ambayo kwa mujibu wa viashiria viliyopo, ni serikali ya wananchi yenye njia tofauti na serikali iliyotangulia, na imefufua matumaini ya wananchi.

Ameyataja mapambano makubwa dhidi ya virusi vya corona na kupungua kwa kiwango kikubwa vifo vya waathiriwa kutokana na utoaji wa chanjo kwa umma kuwa ni miongoni mwa hekaheka za mwaka 1400 Hijria Shamsia na kueleza kuwa, katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia kumefanyika kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kutengeneza chanjo zenye hadhi na kurusha satalaiti katika anga za mbali. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kukiri kwa Wamarekani kwamba wameshindwa kwa fedheha katika mashinikizo yao ya juu kabisa dhidi ya Iran kuwa ni miongoni mwa matukio mengine ya kufurahisha katika upeo wa dunia katika mwaka uliomaliza jana wa 1400 na kuongeza kuwa: Muqawama na kusimama kidete wananchi umepelekea kupatikana ushindi huo, na kwa hakika taifa ndilo lililoshinda.

Ayatullah Khamenei amelitaja suala la hali ngumu ya maisha ya wananchi na mfumuko wa bei kuwa ndilo lililokuwa suala chungu zaidi la mwaka 1400 na kuongeza kuwa: "Matatizo ya kiuchumi yanatibika na ni lazima yapatiwe matibabu na kusema, tunatarajia kuwa baadhi ya matatizo hayo wataondolewa katika mwaka mpya, ambao ni mwaka wa kwanza wa karne ya 15 Hijria Shamsia.

Akieleza sababu ya kutilia mkazo suala la uzalishaji katika miaka ya hivi karibuni Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Uzalishaji ndio ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi na njia kuu ya kuvuka matatizo ya hayo.  

 

3478248/

captcha