IQNA

Rais wa Iran: Waislamu wataungana kwa baraka za Mwezi wa Ramadhani

0:38 - April 04, 2022
Habari ID: 3475092
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe wa salamu za Ramadhan viongozi wa nchi za Kiislamu duniani huku akiwa na matumaini kuwa, kwa baraka za mwezi huu mtukufu Waislamu duniani wataungana.

Katika ujumbe wake huo, Sayyid Raisi amesema: Harufu nzuri ya Ramadhani imetujia tena, ili katika mwezi huu mtukufu, mwezi wa kuteremshwa Qurani tukufu, ambapo makadirio ya mwanadamu huanishwa kwenye Usiku wa Cheo, ni fursa kwa Waislamu na waja wema wa Allah kuimarisha uchaji-Mungu, kujiepusha na madhambi, kuvuna thawabu, na kutakasa mioyo, ili kujikurubisha zaidi kwa Mola.

Rais Raisi amesema anatumai kwa baraka za mwezi huu mtukufu wa rehema, msamaha na baraka, na kwa jitihada za viongozi na wanafikra katika nchi za Kiislamu, umma wa Kiislamu utaungana na kushikamana zaidi.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito wa kuungana ulimwengu wa Kiislamu, kwa kujiweka mbali na mawimbi ya mifarakano, ugaidi wa kitakfiri na misimamo mikali; na kuwa na misimamo ya pamoja katika kupambana na machafuko na kukabiliana na siasa za kiistikbari na mabeberu wa dunia.

Vile vile Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaombea taufiki, mafanikio, ustawi, ufanisi na furaha tele Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu wa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Baadhi ya mataifa ya Kiislamu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq na Oman yametangaza kuwa, leo Jumapili ndiyo siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hata hivyo baadhi ya nchi kama Indonesia, Uturuki, Mauritania, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar, Kuwait, Palestina, na Misri zilianza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani jana Jumamosi.

3478323/

captcha