IQNA

Mkuu wa RTVE Uhispania amkosoa Mkurugenzi wa Eurovision kwa ukimya Kuhusu Gaza

16:22 - December 13, 2025
Habari ID: 3481653
IQNA – Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Umma nchini Uhispania (RTVE), José Pablo López, amemkemea Mkurugenzi wa Mashindano ya Muziki ya Eurovision kwa barua yake ya wazi kwa mashabiki ambayo haikutaja Gaza wala utawala wa Israel, akisema hatua hiyo ni “kushindwa” wakati mashindano hayo yanapitia mgogoro mkubwa wa kiheshima.

López alimshutumu Martin Green, Mkurugenzi wa Eurovision, kwa kutoa ujumbe ambao haukugusia kabisa vita vinavyoendelea Gaza, licha ya kile alichokiita “mgogoro mbaya zaidi wa kiheshima katika historia ya Umoja wa Vyombo vya Utangazaji Ulaya (EBU).”

Barua hiyo ilitolewa wakati mvutano ukizidi kuongezeka, huku mashirika matano ya utangazaji, Uhispania, Uholanzi, Slovenia, Ireland na Iceland, yakijiondoa kushiriki mashindano hayo kupinga ushiriki wa Israel wakati wa vita vya Gaza.

López alisema ujumbe wa Green “umeshindwa kabisa kutambua uzito wa hali halisi.”

Alinukuliwa akisema kwenye mtandao wa kijamii X kwamba:

“Green hataji Gaza wala Israel. Anazungumzia ‘matukio’ Mashariki ya Kati yaliyomgusa. Je, mauaji ya halaiki ni ‘tukio’ tu?”

Akaongeza kuwa faraja kuu ambayo Green aliwapa mashabiki ni kudai kuwa “anasikiliza,” akisema:

“Inaonekana kusikiliza ndilo jukumu lake lote.”

López pia alikosoa kauli ya Green kwamba “yaliyopita si ndwele” na kwamba kuanzia sasa kanuni za mashindano zitatekelezwa ipasavyo.

Akauliza:

“Vipi kuhusu ukiukaji wa kanuni uliofanywa na Israel katika miaka miwili iliyopita? Je, vimefagiliwa tu chini ya zulia?”

Akahoji iwapo EBU inatekeleza kanuni zake “kulingana na maslahi ya kisiasa na kiuchumi.”

Aidha, alikumbusha kuwa siku hiyo hiyo kanuni mpya zilipopitishwa, maafisa wa Israel walidai hadharani kuwa waliwashawishi wajumbe wa nchi mbalimbali kisiasa ili kuhakikisha nchi yao inaendelea kushiriki mashindano hayo.

“Ni nini kingine tutashuhudia?” López aliuliza.

Katika barua yake, Green aliandika kuwa mashabiki wengi wanataka Eurovision ichukue msimamo wa wazi kuhusu masuala ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa njia pekee ya mashindano hayo “kuendelea kuwaleta watu pamoja” ni kuongozwa kwanza na kanuni zake.

Hivi karibuni, wanachama wa EBU walikataa kupiga kura kuhusu ushiriki wa Israel katika mashindano ya 2026, hatua iliyomaanisha kuwa utawala huo katili utaendelea kubaki.

Kutokana na hilo, mashirika matano ya utangazaji—RTVE ya Uhispania, NPO ya Uholanzi, RTVSLO ya Slovenia, RTE ya Ireland na RUV ya Iceland—yakatangaza kususia na kujiondoa kwenye Eurovision kama ishara ya kupinga uamuzi huo.

Habari zinazohusiana
captcha