Sheikh Yasser Qalibo, aliyekuwa na sauti mashuhuri katika kuitisha Adhana na kusoma Qur’ani, na ambaye alisimama imara kulilinda eneo la Al‑Aqsa dhidi ya uvamizi wa Wazayuni, alifariki Ijumaa (Desemba 12).
Katika maisha yake yote, alikuwa mtu wa kudumu ndani ya Msikiti wa Al‑Aqsa, akishiriki katika durusu na vikao vya usomaji wa Qur’ani katika eneo hilo tukufu.
Alikuwa miongoni mwa wakazi mashuhuri wa al‑Quds na Palestina waliopata elimu katika Chuo Kikuu cha Al‑Azhar.
Sheikh Yasser hakuwa tu muadhini na qari wa kawaida, bali alihesabiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na watu wa dini waliounganishwa moja kwa moja na jina la Msikiti wa Al‑Aqsa.
Alikuwa akisoma Qur’ani na kuadhini kwa sauti tulivu, yenye unyenyekevu na utulivu wa kiroho, na maelfu ya waumini wa Palestina walizoea kuisikia sauti yake wakati wa sala na katika hafla mbalimbali za kidini ndani ya Msikiti wa Al‑Aqsa.
Qari na muadhini huyu alijulikana kwa kujitoa kwake bila kuchoka kwa ajili ya Msikiti wa Al‑Aqsa, jambo lililomfanya kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya kiibada ya waumini, licha ya mazingira magumu na changamoto za kiusalama katika eneo hilo.
Sheikh Yasser Qalibo alizaliwa na kukulia katika mazingira ya elimu ya dini. Katika maisha yake yote, alishiriki katika mikusanyiko ya kidini, na uwepo wake katika viwanja vya Msikiti wa Al‑Aqsa ulikuwa ushahidi wa ikhlasi yake katika kulitumikia dini yake na jamii yake.
3495729