
Tarehe 9 Desemba 2025 ilitimiza miaka tisa tangu kufariki kwa Sheikh Radhi, mmoja wa maqari wakubwa wa Idhaa ya Qur’ani ya Misri, mzaliwa wa kijiji cha Shabramant katika eneo la Abu Al-Nimris, mkoa wa Giza, kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Al‑Watan.
Qari huyu wa Misri alifariki dunia mnamo Desemba 9, 2016, baada ya maisha marefu ya kuhudumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na akawaacha wasikilizaji na wapenda Qur’ani na hazina ya tilawa zinazodumu milele.
Kwa kumbukizi ya siku hii, Idhaa ya Qur’ani ya Misri ilirushwa hewani tilawa zake ili kuendeleza njia yake ya Qur’ani na kuenzi mchango wake.
Sheikh Radhi alizaliwa Julai 1, 1936 katika kijiji cha Shabramant, na shughuli zake za Qur’ani zilianza katika Maktab ya kijiji, chuo cha kitamaduni cha kuhifadhisha Qur’ani.
Kwa juhudi kubwa na kipaji cha kumbukumbu kisicho na kifani, alihifadhi Qur’ani yote akiwa na umri wa miaka tisa tu. Hapo ndipo safari yake ya Qur’ani ilipoanza, safari iliyokuja kusikika na kuheshimiwa kote katika ulimwengu wa Kiislamu miongo kadhaa baadaye.
Alikuwa akiamini kuwa Maktab ndizo “mama wa shule zote” za kuhifadhisha Qur’ani, kwa sababu ya roho ya ushindani na bidii miongoni mwa wanafunzi. Aliendelea kuzisifu taasisi hizi hadi siku za mwisho za uhai wake.
Sheikh Radhi pia alimsaidia mwalimu wake kuwafundisha watoto, na idadi ya wanafunzi aliowahudumia ilifikia mia sita. Kila siku, alikuwa mtu wa mwisho kuondoka Maktab.
Kujiunga kwake na idhaa hakukuwa jambo alilolipanga, bali lilitokana na kipaji chake. Katika moja ya makongamano ya kidini aliyokuwa akisoma Qur’ani, Mahmoud Hassan Ismail, aliyekuwa Mkuu wa Idhaa ya Misri wakati huo, alisikia tilawa yake na kushangazwa na upekee wa sauti yake.
Mkuu huyo wa idhaa alimuuliza moja kwa moja kwa nini hakuwahi kuomba kufanya jaribio la kujiunga na idhaa. Ndipo akamwandikia mwenyewe ombi hilo, na Sheikh Radhi akakubaliwa rasmi kuwa qari wa Idhaa ya Qur’ani Tukufu mwaka 1975, akiwa na umri wa miaka 45.
Sheikh Mustafa Ismail ndiye aliyekuwa kigezo chake cha kwanza katika usomaji. Baadaye, Sheikh Radhi aliona kuwa sauti yake ilikuwa karibu zaidi na mtindo wa Sheikh Kamil Yusuf Al‑Bahtimi. Hivyo akaifuata njia yake, huku akidumisha mtindo wake binafsi, mtindo uliotambulika kwa unyenyekevu, uzuri wa makam na ladha tamu ya tilawa.
Mnamo Desemba 9, 2016, wananchi wa Misri na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla walimpoteza mmoja wa nyuso muhimu za usomaji wa Qur’ani kupitia redio. Alifariki akiwa na umri wa miaka 80, na akaacha urithi mkubwa wa tilawa na vikao vya Qur’ani vinavyoendelea kusimulia safari yake ya kiroho.
Katika kumbukizi ya mwaka wa tisa wa kifo chake, wasikilizaji wanaukumbuka ule utamu wa sauti yake, sauti ambayo bado inasikika kupitia Idhaa ya Qur’ani ya Misri; sauti ya mtu aliyekuwa mfano wa qari mnyenyekevu, mwenye heshima na mwenye mapenzi makubwa kwa Qur’ani. Kwa sababu hii, watu walimpenda sana.
3495727