
Taasisi hii inajulikana kama Kituo cha I.M.A.M., kifupi cha Imam Mahdi Association of Marjaeya. Ni ofisi rasmi ya uwakilishi wa Ayatullah Sayyid Ali al‑Sistani, katika bara la Amerika Kaskazini. Ayatullah Sistani mmoja wa wanazuoni wanaofuatwa zaidi katika ulimwengu wa Kishia yaani Marjaa Taqlid.
Kwa zaidi ya miongo miwili, kituo hiki kimekuwa daraja kati ya marja‘iyya na jamii za Kishia zilizotawanyika Marekani na Kanada.
Kazi zake ni za kiutawala, kielimu na kijamii. Taasisi inalenga kutoa mwongozo wa kidini, kuimarisha taasisi za jamii, na kujenga uwezo wa muda mrefu kwa Waislamu wa Kishia wanaoishi katika mazingira ya Magharibi.
Kituo hiki kinaongozwa na Sayyid Mohammad Baqir al‑Kashmiri, mwakilishi wa Ayatullah Sayyid Ali al‑Sistani.
Makao makuu ya I.M.A.M. yako Dearborn, jiji linalotambulika kuwa na miongoni mwa idadi kubwa zaidi ya Waislamu nchini Marekani. Ndani ya jamii hiyo, Waislamu wa Kishia ni sehemu muhimu, wakiwa na mizizi ya muda mrefu miongoni mwa Waarabu, hususan wenye asili ya Lebanon na Iraq.
Uamuzi wa kuanzisha kituo Dearborn haukuwa wa bahati nasibu. Ulilenga kujikita ndani ya jamii ambayo tayari ilikuwa na uhai wa kidini wa Kishia. Badala ya kuanzisha kitu kipya katika mazingira yasiyokuwa na msingi, taasisi ilijenga uwepo wake mahali ambapo misikiti, hawzah, familia na taasisi za kijamii zilikuwa tayari zinafanya kazi.
Kutoka katika kitovu hiki, shughuli za kituo zimeenea hadi maeneo yote ya Amerika Kaskazini, zikihudumia hata jamii ndogo ndogo na zilizotawanyika ambazo mara nyingi hukosa fursa ya kuwasiliana moja kwa moja na taasisi za juu za kidini.
Huduma za Kidini na Kifedha
Miongoni mwa majukumu yanayoonekana zaidi ya Kituo cha I.M.A.M. ni kuwezesha utekelezaji wa wajibu wa kifedha wa kidini, hususan ulipaji wa khums.
Kituo kinawawezesha waumini wa Marekani, Kanada na maeneo mengine kulipa khums na michango ya kidini mtandaoni. Risiti rasmi hutolewa kwa njia ya kielektroniki, na hivyo kuweka mfumo ulio wazi na wenye ufuatiliaji.
Mfumo huu umekuwa njia muhimu inayowaunganisha Waislamu wa Kishia wa Amerika Kaskazini na marja‘iyya katika utekelezaji wa ibada zao.
Elimu: Hawza ya Mufid
Sehemu muhimu ya dira ya I.M.A.M. ni elimu. Hili linaonekana wazi kupitia uungaji mkono wake kwa Mufid Seminary, taasisi ya elimu ya Kishia inayofundisha kwa Kiingereza, yenye makao yake Virginia, karibu na Washington, D.C.
Hawza hii inalenga kukuza wanazuoni wanaoweza kuunganisha urithi wa Kiislamu na mijadala ya kielimu ya Magharibi.
Taasisi inatoa programu za ngazi ya shahada na uzamili, kwa njia ya masomo ya ana kwa ana na masomo ya mtandaoni.
I.M.A.M. pia inajihusisha na uchapishaji, ikitoa vitabu vifupi na rahisi kusomeka kwa lugha ya Kiingereza.
Ushiriki wa Kitaaluma: Mkutano wa AAR
Miongoni mwa maeneo yanayoonekana zaidi ya ushiriki wake wa kijamii ni uwepo wake wa kila mwaka katika mkutano wa American Academy of Religion (AAR).
Kwa miaka mitatu mfululizo, kituo kimekuwa na banda katika maonyesho makubwa ya vitabu ya mkutano huo.
Mkutano wa AAR ndiyo mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa watafiti wa masomo ya dini, ukivutia maelfu ya wataalamu na wachapishaji wakuu wa vyuo vikuu.
Uratibu wa Kidini na Huduma za Habari
Kituo cha I.M.A.M. kina uhusiano wa karibu na Baraza la Maulamaa wa Kishia Amerika Kaskazini, chombo kinachoratibu masuala ya kidini kama vile kuandama kwa mwezi, kalenda ya Kiislamu, na matukio makubwa ya kidini barani humo.
Kalenda na matangazo rasmi ya baraza hilo hupatikana kupitia tovuti ya I.M.A.M.
Kituo kinaendesha tovuti yenye taarifa nyingi, ikitoa mwongozo wa kidini, huduma za michango, kalenda na taarifa za taasisi.
Tovuti hii inakamilishwa na kituo cha YouTube kinachochapisha video fupi za elimu kuhusu hukumu za kidini na maadili.
3495723