IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Kenya yaanza

14:58 - December 01, 2025
Habari ID: 3481601
IQNA – Fainali ya mashindano ya kimataifa kuhifadhi Qur’ani kwa wanaume imeanza leo jijini Nairobi, Kenya.

Katika hafla ya ufunguzi, qari maarufu wa kimataifa wa Qur’ani, Sheikh Abdirashid Ali Sufi, aliwahimiza vijana kuimarisha uhusiano wao na Qur'ani Tukufu, akibainisha kuwa mafundisho yake yanaweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha ya kisasa na kuwahamasisha kuwa wachangiaji wema katika jamii.

“Qur’ani ni mwongozo wetu wa mwisho. Ni muhimu kwa vijana kuikumbatia, kwani ina athari kubwa katika maisha,” alisema.

Akinukuu hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) inayowasifu wanaojifunza Qur’ani na kuwafundisha wengine, Sheikh Abdirashid alisisitiza kuwa kwa kuziishi fadhila za Qur’ani, vijana wanapata nafasi adhimu ya kufanikisha malengo yao na kustawi katika jitihada zao.

Kauli hizi zilitolewa wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Sheikh Ali Sufi toleo la 4, yaliyofanyika katika Sir Ali Muslim Club, Nairobi.

Katika hotuba kuu, Waziri wa Afya Kenya Aden Duale aliwahimiza Waislamu kushikamana na mafundisho ya Qur’ani na kuyaishi maadili yake katika kila nyanja ya maisha. Alisema:

“Mashindano haya yanakusudia kuhamasisha amani, mshikamano na ukuaji wa kiroho kupitia uzuri wa Qur’ani Tukufu.”

Balozi wa Somalia nchini Kenya, Jibril Ahmad Abdulle, naye alisisitiza umuhimu wa kushikamana na mafundisho ya Qur’ani, akieleza kuwa Kitabu Kitukufu ni ushahidi wa imani na nidhamu ya ibada inayowaongoza Waislamu katika kila sura ya maisha.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM), Al Haj Hassan Ole Naado, amesema kuwa Qur’ani ni hazina ya maarifa na urithi mtukufu ambao Waislamu wanapaswa kuukumbatia ili kufanikisha maisha katika nyanja zote.

Mashindano ya mwaka huu yamevutia washiriki 30 kutoka nchi 20 barani Afrika, Ulaya, Asia na Amerika. Katika kipindi cha wiki hii, washindani wataonyesha ustadi wao wa kuhifadhi na kusoma Qur’ani mbele ya jopo la majaji sita mashuhuri.

Miongoni mwa wageni mashuhuri walihudhuria Profesa Ahmed Issa Al-Ma’sarawi kutoka Misri, Sheikh Dr. Waleed bin Idrees Al-Maneese kutoka Marekani, na Sheikh Prof. Sohail Mohammed Iqbal, pamoja na wanazuoni wengine wa Kiislamu.

Mashindano haya ya siku nne yatakamilika kwa kumpa mshindi zawadi ya dola 20,000 za Marekani.

3495574

captcha