IQNA

Makundi ya haki za binadamu, wakazi walaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur’ani Texas

19:14 - December 14, 2025
Habari ID: 3481659
IQNA – Kitendo cha kudhalilisha na kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichotokea mjini Plano, jimbo la Texas, Marekani, kimezua hasira kubwa miongoni mwa wananchi na mashirika ya haki za binadamu.

Katika maandamano yenye utata mjini Plano, mgombea wa Seneti wa chama cha Republican kutoka Florida, Jake Lang, alifanya kitendo cha kuikashifu Qur’ani Tukufu, kwa mujibu wa tovuti ya elmanshar.com..

Katika hatua ya uchochezi, aliweka nakala ya Qur’ani katika kinywa cha nguruwe wakati wa maandamano hayo, kitendo kilichowakasirisha Waislamu, wanaharakati wa haki za binadamu, na wadau wa kimataifa, na kusababisha mshtuko mkubwa ndani na nje ya Marekani.

Katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Lang alionekana amembeba nguruwe mdogo akiwa na Qur’ani mdomoni, akimtaja mnyama huyo kuwa “udhaifu wa Uislamu” na akisema: “Huu ndio udhaifu wenu, Waislamu. Tutawarudisha mlipotoka, tukibeba nguruwe mikononi na Kristo mioyoni mwetu.”

Lang aliandaa maandamano hayo mjini Plano baada ya kufanya matukio mengine kama hayo, ikiwemo lile la Dearborn, Michigan, akidai kuwa ni sehemu ya kampeni yake dhidi ya kile anachokiita “Kuenezwa Uislamu Amerika.”

Wanaharakati waliripoti kuwa maandamano hayo yalielekea katika Jumba la Jiji la Plano yakisindikizwa na kauli chochezi dhidi ya Uislamu.

Hatua hiyo ilizua hasira kali kutoka kwa jamii ya eneo hilo na mashirika ya haki za binadamu, ambayo yaliitaja kama kitendo cha kuchochea chuki ya kidini na kusisitiza kuwa vitendo kama hivyo havichangii mjadala wowote wa kimaadili au kitamaduni kuhusu dini au jamii.

Tukio hilo pia liliibua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii, ambapo watumiaji walishiriki video hiyo na kulikosoa kitendo hicho kama uchochezi wa wazi na dharau kwa hisia za mamilioni ya Waislamu nchini Marekani na duniani kote.

Tukio hili linakuja wakati ambapo ongezeko la maandamano ya chuki dhidi ya Uislamu katika baadhi ya majimbo ya Marekani limewafanya wataalamu wa jamii za kiraia kutoa wito wa kuimarisha juhudi za kuelimisha umma kuhusu madhara ya chuki ya kidini na kuimarisha sheria dhidi ya uchochezi wa vurugu na chuki.

3495730

Habari zinazohusiana
captcha