IQNA

Kadhia ya Nyuklia

Misimamo isiyo sahihi ya IAEA kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran

21:43 - June 09, 2022
Habari ID: 3475356
TEHRAN (IQNA)- Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA jana Jumanne alifanyiwa mahojiano makao makuu ya wakala huo mjini Vienna; na moja ya masuali aliyoulizwa ni kuhusu takwa la Iran la kumtaka alaani hujuma zilizofanywa dhidi ya vituo vyake vya nyuklia.

Grossi alijibu hivi suali hilo: "katika minasaba tofauti nimekuwa nikilaani waziwazi hatua yoyote ya utumiaji mabavu dhidi ya mtu yeyote". Akaendelea kusema: "mimi ni mwanadiplomasia na ninapigania amani; na ninalaani hatua yoyote ya utumiaji mabavu ifanywayo popote na mtu yeyote."

Msimamo huo hafifu na dhaifu wa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuhusuu hujuma na uharibifu uliofanywa kwenye vituo vya nyuklia vya Iran na vilevile kuuliwa kwa wanasayansi na wataalamu wake wa nyuklia unaonyesha kuwa si tu Grossi hajachukua na wala hatachukua hatua athirifu na ya maana juu ya suala hilo, lakini ilivyo hasa ni kwamba, matamshi yake hayo yasiyo na maana yoyote yameupa baraka kamili utawala wa Kizayuni wa Israel za kuendeleza hatua zake hizo ovu na za ukiukaji wa sheria.

Kwa upande mwingine, Rafael Grossi ameashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba, kutekelezwa takwa hilo la Iran la kulaaniwa hujuma zilizofanywa dhidi ya vituo vyake vya nyuklia kunategemea ushirikiano mkubwa zaidi itakaotoa, ambao kwa hakika ni kukubali kutekeleza kila utakachotaka wakala wa atomiki. Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA ameashiria matatizo yaliyozungumziwa na Iran na akasema: "matatizo haya yatatatuliwa pale kila kitu kitakapowekwa wazi; na hapo ndipo Iran itaweza kupata kwa urahisi zaidi mashirikiano inayotaka ipatiwe."

Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ndiye adui mkubwa zaidi wa Iran katika ukanda huu, umekuwa ukisisitiza kila mara kuwa unapinga shughuli za nyuklia za Tehran zenye malengo ya amani; na si tu umekuwa kila baada ya muda ukitoa vitisho vya kufanya mashambulio ya anga dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, lakini pia umeshafanya mashambulio na hujuma kadhaa za uharibifu dhidi ya vituo hivyo. Miongoni mwa hujuma hizo ni ile ya Aprili 10, 2021 iliyofanywa dhidi ya kituo cha nyuklia cha Natanz, ambapo Israel ilitambulika rasmi kuwa ndio iliyohusika. Kabla ya hapo, mnamo tarehe 3 Julai, 2020 msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran aliripoti kutokea "ajali" ndani ya kituo cha kufungia mashinepewa (centrifuges) kwenye kituo hicho cha nyuklia cha Natanz, ajali ambayo ilikuja kubainika baadaye kuwa ni shambulio dhidi ya kituo cha atomiki cha Iran. Hujuma na uharibifu huo vilitilia mkazo kwa mara nyingine tena ulazima wa IAEA kuonyesha msimamo na kuchukua hatua, kwa kuwa ndiyo taasisi angalizi ya kimataifa ya masuala na shughuli za nyuklia za nchi zote wanachama.

Ukweli ni kuwa, kati ya nchi zenye miradi ya nyuklia duniani, Iran ni moja ya nchi chache kabisa ambayo imetishiwa na kushambuliwa mara kadhaa vituo na mitambo yake ya nyuklia. Utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao una ghala kubwa la silaha za nyuklia, kila mara umekuwa ukisisitiza kuwa utakabiliana na nguvu za nyuklia za Iran.

Mbali na hujuma mtawalia za kigaidi ulizofanya za kuwaua wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Iran, ya karibuni kabisa ikiwa ni ya mwaka 2020 ulipomuua shahidi Mohsen Fakhrizadeh, katika miaka ya karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukipanga na kutekeleza kila mara aina mbalimbali za hujuma za intaneti na za moja kwa moja dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Miongoni mwa hujuma hizo za intaneti ni ile iliyofanywa kwa ushirikiano wa utawala haramu wa Israel na Marekani dhidi ya kituo cha nyuklia cha Natanz kwa kutumia kirusi cha Stuxnet.

Miaka michache baadaye, yaani mnamo mwezi Julai 2020, ulitokea mripuko kwenye sehemu ya ufungaji mashinepewa kwenye kituo cha Natanz, ambapo mbali na vyombo vya habari, hata wataalamu wa Kizayuni pia walikiri kuhusika na hujuma hiyo. Wakati ule, Kazem Gharib Abadi, aliyekuwa balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran wakati huo katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna alihutubia kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa na Nishati ya Atomiki na kutangaza kuwa, mripuko huo ulitokana na hujuma ya uharibifu na akatoa mwito kwa wakala huo wa IAEA na wanachama wake walaani vikali kitendo hicho kiovu.

Gharib Abadi alisema: Katika maazimio mbalimbali ya mkutano mkuu wa IAEA imesisitizwa kuwa "shambulio la aina yoyote la utumiaji silaha na vitisho dhidi ya kituo chochote cha nyuklia ambacho ni maalumu kwa shughuli zamani na kiko chini usimamizi wa IAEA, vinachukuliwa kuwa ni ukiukaji wa misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na Hati ya IAEA." Hata hivyo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Mkurugenzi Mkuu wake Rafael Grossi walikataa kutoa tamko lolote la kulaani hujuma hiyo.

Ukweli wa mambo ni kuwa Grossi anaelewa fika kwamba hujuma za uharibifu dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran zinakiuka sheria na kanuni za IAEA na zinapingana waziwazi na sheria za kimataifa. Lakini kinyume na anavyodai kwamba msimamo wa Wakala wa atomiki na yeye mwenyewe binafsi ni wa kutopendelea upande wowote, msimamo wao kwa hatua za aina hiyo za uvunjaji sheria zilizochukuliwa na utawala wa Kizayuni, umekuwa ni kunyamazia kimya kinachomaanisha kuridhia pia.

3479236

Kishikizo: iran IAEA nyuklia
captcha