IQNA

Spika wa Bunge la Iran
17:59 - June 21, 2020
News ID: 3472884
TEHRAN (IQNA) - Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, ametoa kauli baada ya Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kupitisha azimio dhidi ya Iran na kusema: "Nchi za Magharibi na hasa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa mara nyingine tena zimedhihirisha utambulisho wao hasimu na wa kutoaminika mbele ya taifa la Iran."

Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo leo asubuhi katika kikao cha bunge na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya ziko sawa na Marekani katika chuki na uhasama dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: "Kupitishwa azimio la kisiasa katika Bodi ya Magavana ya IAEA dhidi ya Iran ni mpango wa kitoto ulioratibiwa na Wazayuni."

Katika kikao chake cha Ijumaa, Bodi ya Magavana ya IAEA ilipasisha azimio lililopendekezwa na Uingereza, Ujerumani, Ufaransa yaani Troika ya Ulaya,  ambalo limedai kuwa Iran haifungamani na ahadi zake kwa wakala huo.

Spika wa Bunge la Iran amesema Iran itatoa jibu lake kufuatia azimio hilo na kuongeza kuwa, watakaobeba dhima ya kuibua taharuki katika uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni wale waliowasilisha azimio hilo.

Qalibaf ameashiria pia uhusiano mzuri wa Iran na IAEA ambao umedumu kwa muda mrefu na kusema historia ya miaka 17 iliyopita imeonyesha kuwa Iran daima imekuwa ikitekeleza shughuli zake za nyuklia kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maslahi yake ya kitaifa. Ameongeza kuwa Iran imekuwa na uhusiano wa juu zaidi na IAEA lakini haijapata chochote isipokuwa kuzidishiwa uhasama.

Spika wa Bunge la Iran aidha amesisitiza kuwa, mapambano na muqawama wenye busara ambao unaungwa mkono na taifa ambalo limeungana ni chaguo la kistratijia la Iran. Hali kadhalika Qalibaf amesema Iran katu haitafanya mazungumzo na Marekani na kuongeza kuwa, mazungumzo na nchi zingine za Magharibi yatafanyika kwa msingi wa kutoziamini.

3905896

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: