IQNA

Rais Hassan Rouhani
20:26 - June 24, 2020
News ID: 3472893
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema moja ya fahari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa inawaruhusu wanawake waendeleze harakati zao katika sekta mbali mbali.

Akizungumza Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri, Rais Rouhani ametuma salamu za pongezi kwa mnasaba wa 'Siku ya Kitaifa ya Msichana' nchini Iran na kuongeza kuwa Uislamu hauwabagui wanawake.

Amesema baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mazingira mazuri yaliibuka ili kuwawezesha wanawake kujishughulisha katika sekta za sayansi, utafiti na uzalishaji. Aidha amesema leo wasichana wa Iran wamejaa katika vyuo vikuu na wanaohitimu wanafanya kazi katika mahospitali, viwanda, idara za serikali na kadhalika. 

Kwingineko katika hotuba yake, Rais Rouhani ameashiria matatizo yaliyoko katika jamii na kusema ni jukumu la serikali kuyatatua.

Ameongeza kuwa, matatizo yaliyoko hivi sasa yanatokana na janga la COVID-19 ambalo liliibuka miezi michache iliyopita na pia vikwazo vya kidhalimu vya Marekani. Amesema Iran imekuwa ikikabiliwa na vikwazo shadidi kwa muda wa miaka mitatu sasa na kuongeza kuwa maafisa wa serikali wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa matatizo yanatatuliwa.

Kwingineko katika kikao hicho, rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria azimio lililotolewa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Iran na kueleza kuwa: Wakala huo unapasa kubakia katika mkondo wake wa kisheria kwa kulinda uhuru kujitawala kwake mkabala na mashinikio ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Rouhani ameongeza kuwa,Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani zitaka kuuondoa wakala wa IAEA katika majukumu yake makuu kwa kuibua kadhia ya karibu miaka 20 iliyopita. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kulinda nafasi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia kuna umuhimu mkubwa kwa ajili ya mfumo wa kimataifa n a kusisitiza kuwa, msingi wa kazi wa Iran ni kushirikiana na wakala wa IAEA, hata hivyo iwapo italazimika Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali kwa mienendo isiyofaa ya wakala huo.  

Rais Rouhani ameashiria ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia zinazosisitiza kuwa Iran imeheshimu na kutekeleza majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA na kuongeza kuwa: Iran ingali ipo tayari kukubali usimamizi wa kisheria wa wakala wa IAEA katika fremu ya taratibu zilizopo na kushirikiana kwa karibu na wakala huo. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia tabia ya kutotekeleza ahadi upande wa Ulaya na kueleza kuwa nchi za Ulaya hazijatekeleza majukumu yao ya kisheria na pia ahadi zao kabla na baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Amesema nchi hizo zinaomba radhi kwa hatua hizo kwa kupiga simu na katika vikao mbalimbali lakini Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na italinda uhuru na kujitawala kwake katika mazingira yaliyosababishwa na utawala wa Kizayuni na Marekani. 

3906675

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: