IQNA

Tafsiri ya Qur’ani na Wafasiri /8

Al-Tibbyan; Tafsiri ya kwanza kamili ya Qur’ani ya mwanazuoni wa Kishia

22:14 - November 21, 2022
Habari ID: 3476123
TEHRAN (IQNA) – Al-Tibbyan Fi Tafsir al-Qur’an iliyoandikwa na Sheikh Tusi ni tafsiri ya kwanza ya Qur’an Tukufu iliyoandikwa na mwanazuoni wa madhehebu ya Shia ambayo inajumuisha Sura zote za Qur’ani.

Tafsiri hiyo inatumia sayansi na nyanja mbalimbali za Qur’ani na halikadhalika nyinginezo kama vile Hadith, Fiqh, theolojia, historia, Sarf na Nahw (sarufi ya Kiarabu).

Muhammad bin Hassan bin Ali bin Hassan, ambaye ni maarufu kwa lakabu ya Sheikh Tusi na Sheikh At-Taeifa, ni miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kishia katika nyanja za Hadithi na Fiqh. Alihama kutoka Khorasan (Iran kaskazini-mashariki ya Iran ya sasa) hadi Iraq akiwa na umri wa miaka 23 kusoma sayansi ya Kiislamu na akajifunza kutoka kwa wanazuoni wakuu kama Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha.

Khalifa wa ukoo wa Bani Abbas, Al-Qaim bi Amrillah, alimpa idhini ya kufundisha Uislamu huko Baghdad. Alishikilia nafasi hiyo hadi Baghdad ilipotekwa na Waturuki wa kaumu ya Seljuk, ambapo kiongozi wa Waturuki hao, Tughril, aliiingia mjini na kuchoma moto maktaba yake.

Kisha Sheikh Tusi akaelekea Najaf na kuendelea na masomo yake na shughuli zake za kielimu huko. Aliweza kuandaa shughuli za kitaaluma katika jiji na kuunda maduara ya masomo. Wanachuoni wengine waliungana naye na punde mji wa Najaf ikawa kituo cha kielimu na kiitikadi cha Waislamu wa Shia na hadhi hiyo imeendelea hadi sasa.

Sheikh Tusi alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Baghdad waliotegemea urazini na mantiki na alifuata na kuikamilisha mbinu ya walimu wake Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha.

Aliandika vitabu katika nyanja mbalimbali za kidini na alikuwa na athari ya kudumu katika fikra ya Kishia kwa vitabu hivi na wanafunzi aliowafundisha. Ijtihad na urazini ulitawala katika Fiqh na imani za Shia kutokana na juhudi zake na kuhitimisha satwa ya itikadhi ya Akhbari iliyotawala karne nyingi. Anajulikana kama mfufuaji wa sayansi ya Usul Fiqh na mwanachuoni wa kwanza aliyesababisha Ijtihad kuingia katika Fiqhi.

 Mbinu ya Tafsiri ya Sheikh Tusi

Kama ilivyoelezwa hapo awali, kitabu Al-Tibbyan Fi Tafsir al-Quran kilikuwa tafsiri ya kwanza ya Qur'ani ya mwanazuoni wa Kishia ambayo inajumuisha aya zote za Quran. Tafsiri za Shia kabla ya Sheikh Tusi zilitaja baadhi tu ya Hadithi katika tafsiri ya aya za Qur’ani. Sheikh Tusi, hata hivyo, alitilia maanani na kusoma maoni ya wanazuoni na wafasiri wote waliotangulia, wawe ni madhehebu ya Shia au Sunni, na maandishi ya fasihi ya Kiarabu yaliyoanzia zama za kabla ya kuja kwa Uislamu.

Miongoni mwa vipengele vingine vya tafsiri yake ni kutoa maelezo kuhusu maneno magumu, tofauti za usomaji, na Fiqh, theolojia, na nukta za balagha.

Baadhi wanaamini kwamba sifa kuu ya njia yake ya kufasiri ni utumizi wa Ijtihadi na muelekeo wa urazini ambao ni tofauti muelekeo unaoegemea Hadith pekee uliofutwa  na wafasiri kabla yake.

Inaonekana kuwa ni tafsiri ya kwanza ambayo mwandishi hakukusanya Hadithi zinazohusiana na Tafsir tu, bali pia alifanya Ijtihad, uhakiki na uchambuzi. Yaani pamoja na kunukuu na kuhakiki Hadithi za Mtume Muhammad SAW na Ahul Bayt AS, na mitazamo na fikra za wafasiri waliotangulia, Sheikh Tusi anatoa maoni yake.

Al-Tibbyan inachukuliwa kuwa tafsiri ya vyanzo vingi au pana. Katika njia hii, mfasiri anatumia vyanzo kama vile Qur’anI, Hadith, na akili katika ufahamu wake wa kufasiri.

Katika ufafanuzi huu, Sheikh Tusi anaanza kufasiri kila Sura kwa kuzungumzia jina la sura, ikiwa ni Makki au Madani, na sifa zake nyingine. Kisha anajadili maana za neno, tofauti za usomaji, Sarf, Nahw na nukta za balagha na kisha kutoa maelezo na kutaja mitazamo tofauti.

Majadiliano yake ya Fiqhi katika kitabu hiki mara nyingi yanatolewa kwa njia ya kulinganisha kati ya shule na madhehebu mbalimbali.

captcha