IQNA

Tafsiri za Qur'ani Tukufu na Wafasiri / 11

‘Min Huda al-Qur'an’; Njia ya kijamii, kielimu ya kufasiri aya za Qur'ani Tukufu

18:33 - December 13, 2022
Habari ID: 3476243
TEHRAN (IQNA) – Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya Min Huda al-Qur'an iliyoandikwa na Ayatullah Seyed Mohammad Taqi Modarresi, mwanazuoni wa Iraq na mfano wa kuigwa, ni miongoni mwa tafsiri za kisasa za Qur'ani Tukufu.

Tafsiri hii imechapishwa katika juzuu 18 na inajadili aya zote za Qur'ani Tukufu kwa mtazamo wa kijamii na kielimu au kisayansi.

Ayatullah  Seyed Mohammad Taqi Modarresi (alizaliwa mwaka wa 1945), ni mwana wa Seyed Mohammad Kadhim Husseini Khorasani Modarres Haeri, ambaye ni mwanazuoni wa Kishia, mwanafikra na mwandishi wa zama hizi. Mfasiri huyu alizaliwa katika mji mtakatifu wa Karbala katika familia ya wanazuoni na mafuqaha.

Alisoma taalamu za kidini na kufaidika na wasomi wakubwa. Pia amesoma taalumu zingine, na kuwa mtaalam katika nyanja kadhaa kama vile falsafa, irfani, na uhakiki wa utamaduni wa Magharibi.

Ameandika makala  nyingi, zilizochapishwa katika majarida na magazeti ya lugha ya Kiarabu huko Iraq, Iran na Lebanon.

Yeye ni mwalimu maarufu wa vyuo vya Kiislamu au Hauza (seminari) na amechukua hatua za kurekebisha Hauza kwa kuleta mbinu mpya kulingana na mahitaji ya kisasa.

Ayatullah Modaressi pia hutoa katika mihadahrai tofauti na hivyo kuongeza ufahamu miongoni mwa watu kuhusu majukumu yao.

 Tafsiri ya Min Huda al-Quran

Katika tafsiri hii ya Qur'ani Tukufu mfululizo wa aya zimetajwa kwanza na baada ya kuashiria ujumbe wa jumla wa aya hizo, kila sehemu ya kila aya inajadiliwa. Kila sehemu imepewa kichwa na ina somo. Mwandishi anazingatia vipengele vya kutafakari na busara katika tafsiri.

Kwa kutumia aya za Qur'ani Tukufu, tafsiri hii inarejelea ukweli wa kijamii na kielimu. Mbinu maalum ya kutafakari iliyotumiwa katika tafsiri hii ina umuhimu mkubwa na kwa mbinu hii, mwandishi anachanganua jinsi ya kuingiliana na hali za kijamii. Pia anajaribu kuepuka masuala tata ambayo si katika mahitaji la dharura  ya harakati ya Kiislamu. Hii ni miongoni mwa nukta zinazotofautisha tafsiri hii na nyinginezo.

Kwa ujumla, kuna njia maalum na ya ubunifu  katika uandishi wa tafsiri hii ya ‘Min Huda al-Qur'an’ . Yaliyomo yametolewa kwa njia rahisi na sahali kuelewa, ya utaratibu na ya kuvutia. Mwandishi harejelei maoni ya wafasiri wengine.

Miongoni mwa vipengele vingine vya tafsiri hii ni matumizi ya uchanganuzi wa kisaikolojia katika kujadili vipengele vya kielimu vya aya. Pia, mwandishi anajaribu kuhusisha maudhui ya aya na hali halisi ya leo na hali ya kiutamaduni, kijamii, na kisiasa ya Umma wa Kiislamu.

Tafsiri hii inalenga katika kueleza dhana za aya na kujadili malengo ya aya hizo na suluhisho zinazotoa kwa changamoto au matatizo katika jamii. Katika tafsiri hii, yaliyomo yametolewa kwa njia iliyoainishwa na mijadala ya kiufundi na kitaaluma mbinu za tafsiri zilizotanguliwa imeepukwa kwa kiasi kikubwa. Madhumuni ya mwandishi, hata anapotaja Hadith, ni kueleza njia ya kielimu na kimaadili ya Qur'ani Tukufu ili  kuzielewa aya kwa kina.

captcha