IQNA

Tafsiri ya Qur'ani 7

Usahihi wa Tafsiri inayonasibishwa na Imam Hassan Askari AS

18:36 - October 12, 2022
Habari ID: 3475920
TEHRAN (IQNA) – Kuna tafsiri ya Qur'ani Tukufu inayonasibishwa kwa Imam Hassan Askari (AS) ambayo imetufikia lakini baadhi ya wanachuoni wanatilia shaka unasibishaji huo.

Pamoja na hayo, kulingana na Ayatollah Ali Akbar Seyfi Mazandarani, kuna sababu mbili zinazothibitisha ukweli katika unasibishaji huo.

Imam Hasan al Askari (AS) ni Imam wa 11 wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia na alizaliwa mwaka 232 Hijria Qamaria mwezi 8 Mfunguo Saba Rabiuth Thani katika mji mtakatifu wa Madina.

Ayatullah Seyfi Mazandarani ameafiki kuwepo tafsiri ya Qur'ani ya Imam Hassan Askari (AS) na hapa chini ni baadhi ya nukta katika hotuba yake katika kikao cha tafsiri ya Qur'ani kuhusiana na kadhia hiyo.

Katika taaluma ya Tafsiri ya Qur'ani Tukufu, tunalo suala la kuaminika na usahihi wa kila riwaya. Kuna tafsiri ya Qur'ani inayonasibishwa na Imam Hassan Askari AS ambayo imetufikia. Ina tafsiri ya Qur'ani hadi aya za mwisho za Sura Al-Baqarah. Baadhi wameibua shaka kuhusu kunasibishwa kwake na Imam Hassan Askari (AS).

Hata hivyo, sababu kuu tunayoamini kuwa ni sahihi ni kwamba mtu mmoja aitwaye Mohammad ibn Qassem Astarabadi, anayejulikana kama Mufassir, ameikusanya. Astarabad ni eneo la Gorgan kaskazini mwa Iran. Astarabadi ni mtu anayeaminika katika historia.

Yeye mwenyewe ananukuu kutoka kwa wapokezi wawili ambao wamezitaja riwaya hizi kutoka kwa Imam Askari (AS). Anawataja kuwa ni Imamiya Shia, maelezo yanayoashiria sifa.

Jambo muhimu hapa ni kwamba kuna sababu nyingine ya uhakika nayo ni ukweli kwamba Sheikh al-Saduq amerejea Hadithi nyingi kutoka katika kitabu hiki katika kazi zake zote.

Marehemu Sheikh al-Saduq alikuwa mwanachuoni mashuhuri aliyeishi karibu na wakati alipoishi Imam Hassan Askari (AS). Baba yake pia alikuwa miongoni mwa masahaba wa karibu wa Imam Askari (AS).

Lau kungekuwa na shaka juu ya usahihi wa kitabu hicho, isingepuuzwa na Sheikh al-Saduq, ambaye alikuwa mtaalamu wa Hadithi. Ni ukweli kwamba ameiamini kazi hiyo na kuinukuu mara kwa mara. Hizi ni dalili ambazo tunasema riwaya za tafsiri ya Imam Hassan Askari AS ni sahihi na tunazitumia katika tafsiri yetu.

captcha