IQNA

Tafsiri ya Qur’ani na Wafasiri /6

Tafsiri ya Qur’ani ambayo haikukamilika

19:22 - November 14, 2022
Habari ID: 3476086
TEHRAN (IQNA) – Sayyid Mostafa Khomeini alikuwa gwiji ambaye alianza kuandika tafsiri ya Qur’ani Tukufu iitwayo “Miftah Ahsan Al-Khazaein al-Ilahiya” lakini aliaga dunia kabla ya kuikamilisha.

Alipata taufiki ya kuandika tafsiri ya Sura Al-Fatiha na baadhi ya aya katika Sura Al-Baqarah.

Kuandika tafsiri ya aya zote za Qur’ani Tukufu ni kazi kubwa inayochukua miaka mingi kukamilika. Ndiyo maana baadhi ya wafasiri walianza kazi hiyo lakini wakaaga dunia kabla ya kuimaliza. Miongoni mwao ni Sayyid Mostafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu- ambaye naye alikuwa ni mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Faqihi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sayyid  Mostafa alikuwa gwiji katika shughuli zake za kielimu. Katika tafsiri yake ya Qur’ani Tukufu, inayoitwa Tafseer Al-Qur’an Al-Kareem na pia inajulikana kama "Miftah Ahsan Al-Khazaein al-Ilahiya", alitoa tafsiri za Sura Al-Fatiha na baadhi ya aya kutoka Surah Al-Baqara.

Sayyid Mostafa (1930-1977) alikuwa mtoto mkubwa wa Imam Khomeini. Alikuwa Mujtaid katika ngazi za kielimu za madhehebu ya Shia na pia miongoni mwa wale waliopigania ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Alisoma na wanazuoni wakubwa kama Imam Khomeini, Ayatullah Boroujerdi, Sayyid Mohammad Mohaqeq Damad, Sayyid Mohammad Hojjat Kouhkamarei, na Ayatullah Khoei, akifikia daraja la Ijtihad akiwa na umri wa miaka 27.

Alijitahidi kwa ajili ya utekelezaji wa kivitendo wazo la serikali ya Kiislamu na akaandika kitabu alichokipa anuani ya “Uislamu na utawala”.

Pamoja na Fiqh na Usul, alisoma falsafa, Hikma, theolojia, mafumbo, unajimu, historia, na tafsiri ya Quran.

Ameandika vitabu vingi katika nyanja tofauti za sayansi ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Tafseer Al-Quran Al-Kareem.

Sayyid Mohammad Mousavi Bojnourdi, ambaye alikuwa mwanafunzi mwenzake katika Hauza (seminari ya Kiislamu), anasema kwamba kama tafsiri hii ya Qur’ani ingekamilika, ingekuwa ya kipekee katika ulimwengu wa Kishia.

Moja ya sifa kuu zinazoitofautisha na tafsiri nyinginezo za Qur’ani ni ufahamu wake. Sayyid  Mostafa, ambaye, kama baba yake, alikuwa mjuzi katika masuala ya utafiti ya kielimu, alikuwa mjuzi katika Fiqh na Usul, erfani, maadili, falsafa, fasihi ya Kiarabu, na sayansi nyinginezo za Kiislamu na kwa kutumia nyanja hizi, aliandika tafsiri kwa mitazamombali mbali.

Umahiri wake juu ya nyanja mbalimbali pia ni dhahiri katika uwezo wake wa kuunganisha mistari na nyanja hizo. Upeo wa kazi hii ni kwamba tafsiri ya Surah Al-Fatihah na aya za kuanzia za Surah Al-Baqarah zimechapishwa katika juzuu tano.

Kwa mujibu wa watafiti wa Tafsiri za Qur’ani, Sayyid Mostafa ametumia njia ya Ijtihadi katika tafsiri hii. Ndiyo maana kila anapokutana na wazo lililojipatia umaarufu kinyume na utafiti, hulitolea uhakiki na kulitolea mwanga kwa sababu za uhakika. Kwa mfano, katika tafsiri tofauti imesemwa kwamba Hamd na Shukr ni maneneo yenye maana sawa, lakini yeye analiita wazo hilo kuwa ni Qareeb (ajabu) na kulijadili kwa pembe mbalimbali.

captcha