IQNA

Viongozi wa HAMAS, Mamlaka ya Ndani ya Palestina watembelea Saudi Arabia

17:29 - April 19, 2023
Habari ID: 3476889
TEHRAN (IQNA)- Ismail Hania na Khalid Mash'al, Mkuu wa sasa na wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS Jumapili ya tarehe 16 Aprili waliwasili Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia wakiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa HAMAS.

Mussa Abu Marzouk, afisa wa mahusiano ya kimataifa na Zaher Jabarin, afisa wa ofisi ya mateka na majeruhi wa vita ni wajumbe wengine wa ngazi za juu wa HAMAS waliongozana na Ismail Hania katika safari hiyo ya Saudia.

Viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina pia akiwemo Rais Mahmoud Abbas wapo nchini Saudia na wanatarajiwa kuweko huko hadi Jumatano ya leo tarehe 19 Aprili. Baadhi ya viongozi walioambatana na Mahmoud Abbas katika safari ya Saudia ni Hussein Sheikh, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na Majid Faraj, Mkuu wa Intelijensia ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Takribani majuma mawili yaliyopita, Saudia ilimualika Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa ajili ya kushiriki katika dhifa ya futari. Hii ni katika hali ambayo, Disemba mwaka jana Mahmoud Abbas hakufanikiwa kukutana na kiongozi yeyote yule rasmi wa Saudia wakati aliposhiriki katika mkutano wa viongozi wa mataifa ya Kiarabu na China uliofanyika nchini Saudia. Kualikwa nchini Saudia ujumbe wa ngazi za juu wa HAMAS na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa uongozi wa Ismail Hania na Mahmoud Abbas ni hatua ambayo inaweza kutathminiwa katika pande kadhaa:

Upande wa kwanza ni kuwa, inaonekana kuwa, Saudia imo mbioni kuwa na uhusiano na viongozi wote wawili wa Palestina ambao wanaongoza harakati tofauti na hasimu huko Palestina.

Uhusiano wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala wa Saudia ulitumbukia nyongo mwaka 2007 kufuatia kusambaratika hati ya makubaliano ya Makka. Ushindi wa chama cha HAMAS katika uchaguzi Bunge huko Palestina uliandaa uwanja wa chama hicho kuwa na mamlaka na udhibiti kwa Ukanda wa Gaza na kutimuliwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika eneo hilo.

Safari ya mwisho ya ujumbe wa Hamas huko Riyadh ilifanyika mwaka 2015 ambapo wakati huo Khalid Mash'al alikuwa Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Katika safari hiyo Mash'al alikutana na kufanya mazungumzo na Mfalme Salman bin Abdul-Aziz wa Saudia pamoja na baadhi ya viongozi wa nchi hiyo.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa taarifa na kusema: Kukurubishwa uhusiano wa kidiplomasia na Saudia, ni hatua moja muhimu katika njia ya umoja wa umma wa Kiislamu na hilo litasaidia kuongeza usalama, uthabiti wa kieneo na maelewano baina ya mataifa ya Kiarabu na serikali za Waislamu.

Taarifa hiyo ya HAMAS imeongeza kuwa, hatua hiyo ni katika fremu ya maslahi ya kadhia ya Palestina na kuunga mkono muqawama mkabala wa uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina na matukufu ya tafa hilo.

Inaonekana kuwa, moja ya matokeo ya kufikia mapatano Saudia na mataifa ya Iran na Syria ya kuboresha uhusiano na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia ni kuandaa uwanja wa kuzipatinisha harakati za Hamas na Fat'h. Hilo mbali na kuwa yatakuwa mafanikio makubwa kwa Palestina na eneo la Asia Magharibi, lakinii hapana shaka kuwa, litakuwa pigo kubwa pia kwa utawala haramu wa Israel.

/3483255

Kishikizo: hamas saudia
captcha