IQNA

Amani

Mabadilishano ya wafungwa Yemen baina ya Ansarullah na waitifaki wa Saudia

22:26 - April 17, 2023
Habari ID: 3476883
TEHRAN (IQNA)-Harakati ya Ansarullah ya Yemen na Baraza la la Urais linaloungwa mkono na Saudi Arabia (PLC) wamewaachilia huru wafungwa wengi katika mabadilishano ya mwisho ya wafungwa 900 na hivyo kuongeza matarajio ya amani ya nchi nzima katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vikali vinavyoongozwa na Saudi Arabia.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), ambayo inasimamia zoezi la kubadilishana wafungwa, imesema kwamba ndege zilizobeba wafungwa walioachiliwa huru zilipaa kwa wakati moja kutoka mji mkuu wa Sana'a na mji wa kaskazini wenye utajiri wa nishati wa Ma'rib.

Mshauri wa vyombo vya habari wa ICRC, Jessica Moussan, alitangaza Jumapili kwamba wafungwa 48 wa zamani walikuwa kwenye ndege ya Ma'rib-Sana'a, wakati wengine 42 walikuwa kwenye ndege ya Sana'a-Ma'rib."

Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema duru ijayo ya mazungumzo na Saudi Arabia itaanza baada ya sikukuu ya Idul-Fitr inayotarajiwa tarehe 21 Aprili.

Mazungumzo ya mwisho yalimalizika saa chache kabla ya wafungwa 318 kusafirishwa kwa ndege nne siku ya Ijumaa kati ya mji wa bandari wa kusini mwa Yemen,  Aden na Sana'a, na kuwaunganisha wafungwa na familia zao.

Siku ya Jumamosi, wafungwa 357 walisafirishwa kwa ndege kati ya mji wa Saudi wa Abha na Sana'a. Wasaudi walikuwa miongoni mwa wafungwa walioachiliwa. Haijajulikana kila upande bado una wafungwa wangapi.

Pande zote katika mzozo wa Yemen zilikubaliana katika mazungumzo nchini Uswizi mwezi uliopita kuwaachilia huru wafungwa 887 wa kivita na kukutana tena mwezi Mei kujadili suala la kuachiliwa huru wafungwa zaidi. Mkataba huo ulisimamiwa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Hans Grundberg, na ICRC.

Ujumbe wa Saudi Arabia siku ya Alhamisi ulihitimisha mazungumzo ya amani mjini Sana’a na maafisa wa harakati ya Ansarullah. Maafisa hao wa Yemen wameyataja kuwa yaliyokuwa na mafanikio na kusema majadiliano zaidi yanahitajika ili kuondoa tofauti zilizosalia.

Saudi Arabia ilianzisha vita vya umwagaji damu dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa ushirikiano na baadhi ya washirika wake na kwa usaidizi wa silaha na vifaa kutoka Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi ili kumrejesha madarakani Abdulrabuh Mansour Hadi, ambaye alijiuzulu wadhifa wake wa urais mwishoni mwa 2014 na baadaye kukimbilia Riyadh.

Lengo la vita lilikuwa kuangamiza harakati ya Ansarullah, ambayo imekuwa likiendesha masuala ya serikali bila ya kuwepo serikali madhubuti nchini Yemen.

Hata hivyo, Saudia sasa inaonekana kutupilia mbali malengo yake yote baada ya kuua makumi ya maelfu ya Wayemeni na kuifanya nchi nzima kuwa eneo la mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

4134787

captcha