IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Licha ya kuenea sana mitandao ya kijamii, umuhimu wa kitabu utaendelea kuwa juu

20:38 - May 14, 2023
Habari ID: 3476999
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwishoni mwa kutembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran kwamba, licha ya kuenea sana mitandao ya kijamii, lakini nafasi na umuhimu wa kitabu utaendelea kuwa juu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili baada ya masaa matatu ya kutembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, maonyesho ya vitabu ya kila mwaka, ni kongamano adhimu la watu ambalo sehemu yake kubwa ni ya masuala ya kiutamaduni na jambo hilo linafurahisha na kutia shauku sana. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, pamoja na kuwepo matatizo mbalimbali ya kiuchumi na mfano wake, lakini idadi ya vitabu vya kila namna imeongezeka.

Aidha amesisitiza kuwa, kazi zote za sanaa, vyombo vya habari na utamaduni kama michezo ya kuigiza, sinema na hata uchoraji na kazi za kusikiliza na kuangalia zinahitajia uwepo wa vitabu na mtu anayeweza kufanya kazi nzuri ya kisanii na ya vyombo vya habari ni yule ambaye haachani na vitabu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo pia uchapishaji wa vitabu vya watoto na vijana wadogo na kuongeza kuwa, inafurahisha kuona kwamba, katika vibanda vingi ameona kuna vitabu vya namna hiyo wakati alipotembelea maonyesho hayo.

Amma kuhusu vitabu vinavyochapishwa kuhusiana na kumbukumbu za vita vya kujihami kutakatifu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  amesema, jambo hilo ni muhimu sana. Amesema, Alhamdulillah wimbi jipya la uzalishaji wa vitabu vya namna hiyo limeanza na waandishi wanawake wamejitokeza kwa wingi zaidi na kalamu zao nazo ni nzuri na za kuvutia sana.

4140721

captcha