Arbaeen ni tukio la kidini ambalo aghalabu huadhimishwa na Waislamu wa madhehebu Shia katika siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na imamu wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Ni miongoni mwa mjumuiko mkubwa zaidi za kila mwaka duniani, huku mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na Masunni wengi na wafuasi wa dini nyinginezo wakitembea kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen iliangukia tarehe 25 Agosti.
Espaliú amekuwa miongoni mwa wageni wa Kikristo wa Arbaeen katika miaka ya hivi karibuni. Akizungumza na IQNA, alisema Arbaeen haikuwa na maana maalum kwake kabla ya kuhudhuria matembezi hayo kwa mara ya kwanza miaka michache iliyopita.
Lakini baada ya kushiriki anasema: “Sikuzote nilitamani kurudi. Sikuwa nimewahi kuona kusanyiko kubwa kama hilo la waumini wakitembea bega kwa bega wakiwa kwa amani.”
Aliongeza kuwa kuwa Mkristo si tatizo, kwani anakaribishwa popote alipokwenda.
Anaongeza kuwa: "Zaidi ya hayo, sikuwa Mkristo peke yangu pale, kwani kulikuwa na wengine kutoka Iraq, Armenia na nchi nyingine walioshiriki katika matembezi hayo."
Espaliú alisema jumbe kuu za hija ya Arbaeen ni pamoja na kujitahidi kwa ajili ya amani ya dunia, kusaidia wanadamu wenzako, na kupigania haki ya kimataifa.
Pia alisisitiza kuwa matembezi ya Arbaeen yanaweza kuwa kielelezo cha kuimarisha umoja na kuishi pamoja kwa amani miongoni mwa wafuasi wa imani mbalimbali.
“Tukio hili linapaswa kukuzwa zaidi kwa wasio Waislamu ili watambue kuwa liko wazi kwa kila mtu. Kwa bahati mbaya, Arbaeen hajulikani sana katika nchi za Magharibi na vyombo vya habari haviangazii ipasavyo.”
Mwandishi Habari na mpiga picha huyo wa Uhispania pia alisema Arbaeen inaweza kusaidia kukuza mabadilishano ya kitamaduni kati ya jamii tofauti, kuzuia upendeleo na kukuza maelewano.
"Watu wengi wa nchi za Magharibi hawana taarifa sahihi kuhusu Uislamu na Ushia, na Arbaeen inaweza kuwa fursa kwao kujifunza zaidi kuhusu dini hiyo."
Arbaeen inaweza kutumika kama njia ya kupanua diplomasia ya kidini na uhusiano mzuri kati ya dini, alisema.
3489839