IQNA

Jeshi la Iran lazuia kwa mafanikio hujuma ya Israel

12:46 - October 26, 2024
Habari ID: 3479645
IQNA - Kikosi cha ulinzi wa anga cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimethibitisha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulio ambayo yamelenga maeneo katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam, na kusema uchokozi huo umezimwa kwa mafanikio.

Katika taarifa iliyotoa mapema leo, Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Iran kimesema: “licha ya maonyo yaliyotolewa na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu kwa utawala wa kihalifu na haramu wa Kizayuni wa kujiepusha na vitendo vyovyote vya chokochoko, utawala huo bandia umeshambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam asubuhi ya leo katika hatua ya kuzusha mvutano”. 
 
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, hata hivyo, Mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi umefanikiwa kuzuia na kuzima kitendo hicho cha uchokozi.
 
Imeelezwa kuwa mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mdogo katika baadhi ya maeneo na uchunguzi unaendelea kufanywa kubaini uzito wa tukio hilo.

Hapo awali, duru za usalama zilisema sauti kubwa zilizosikika na baadhi ya watu karibu na Tehran zilitokana na kuwashwa na kufanya kazi mitambo ya ulinzi wa anga.

Wakati huo huo, Fatemeh Mohajerani, Msemaji wa serikali ya Iran amesema leo Jumamosi kwamba, uharibifu wa mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo ya Israel dhidi ya Iran ni "kiduchu" na kwamba hali ya nchi ni "ya kawaida" na shwari.

Akizungumzia kuenea kwa picha za uongo na ripoti ambazo hazijathibitishwa, Mohajerani amewataka wananchi wa Iran kuwa watulivu na wajiepushe na kuamini uvumi, akiwahimiza kutegemea tu vyombo rasmi vya habari na taarifa kutoka kwa vikosi vya ulinzi wa anga vya Iran kwa na maelezo sahihi.

Mohajerani pia amelipongeza jeshi la anga la Iran kwa hatua yao ya kulinda kwa nguvu maeneo ya kijeshi dhidi ya mashambulio ya Israeli akisisitiza kuwa, hatua hiyo imehuisha fahari ya kitaifa ya Wairani.

3490422

captcha