
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Tijan an Nur yalifanyika mjini Doha wiki iliyopita, Awab alisema.
“Nililiwakilisha Yemen katika mashindano haya. Hatua ya kwanza ya mashindano haya ilihusisha kuwasilisha rekodi za sauti kutoka Yemen kwa kamati ya majaji nchini Qatar. Nilishindana na wenzangu wa Yemen na kushinda, na hivyo nikapata nafasi ya kuwa mwakilishi wa Yemen kwenye mashindano haya.”
Kwa mujibu wa Awab, jopo la majaji lilimwalika kushiriki hatua ya mwisho ya mashindano huko Doha, ambayo yalishirikisha idadi kubwa ya watoto kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13 alielezea mashindano ya Qatar kuwa magumu na changamoto, akisema: “Niliweza kushinda nafasi ya kwanza na kulinua jina la nchi yangu miongoni mwa mataifa mengine duniani.”
Baba yake alisema kuwa mwanaye amekuwa na shauku kubwa ya kujifunza tangu utotoni na ana sauti nzuri. “Alipokuwa na umri wa miaka minane, alihudhuria vikao vya kuhifadhi Qur’ani katika Jumuiya ya Misaada ya Hail Saeed katika mji wa Taiz, Yemen.
“Sambamba na kuhifadhi Qur’ani, kipaji cha mwanangu cha sauti katika kuimba nyimbo za Kiislamu kilijitokeza, na mara kwa mara alipata nafasi za juu katika mashindano ya kuhifadhi Qur’ani na nyimbo za kidini.”
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Tijan an Nur ni mashindano ya kimataifa ya Qur’ani yanayoandaliwa na Televisheni ya Jeem nchini Qatar. Watoto wenye umri wa miaka 9-13 pekee ndio wanaweza kushiriki katika programu hii.
Toleo la hivi karibuni litarushwa na Jeem TV wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.