IQNA

Polisi wa Denmark wachunguza shambulio dhidi ya Msikiti wa Imam Ali (AS)

15:39 - July 22, 2025
Habari ID: 3480982
IQNA – Polisi katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, wameanzisha uchunguzi kuhusiana na shambulio lililofanywa na kundi la vijana wa mrengo mkali dhidi ya Msikiti wa Imam Ali (AS).

Msikiti wa Imam Ali (AS), uliopo katika mtaa wa Norrbro jijini Copenhagen, ulilengwa Ijumaa, Julai 18, na kundi la vijana wa mrengo mkali linalojiita "Generation Identity".

Uongozi wa msikiti huo umelaani tukio hilo, na kulitaja kuwa ni shambulio la wazi dhidi ya haki ya kuabudu kwa amani na kushiriki ibada za kidini.

Katika video iliyosambazwa na kundi hilo kwenye mitandao ya kijamii, vijana wanne waliovaa mavazi ya njano walionekana wakipanda juu ya paa la msikiti asubuhi ya Ijumaa, wakiwa na mabomu ya moshi mekundu na kuonyesha bango lenye maneno: "Sitisheni Kueneza Uislamu; Rudisha Wahamiaji Sasa."

Msemaji wa kundi hilo, Daniel Nordentoff, aliambia gazeti la Denmark Berlingska kwamba lengo la kitendo hicho ni “kuelekeza umakini kwa ukweli kwamba msikiti huu ni alama ya mambo ambayo hayafai kuwepo Denmark.”

Polisi wa Copenhagen wamesema walipokea taarifa juu ya tukio hilo na wanalifanyia uchunguzi, lakini hawakutoa maelezo zaidi.

Msemaji wa kundi hilo la siasa kali alisema tukio hilo halikusababisha uharibifu wa mali yoyote na lilidumu kwa dakika kumi tu:“Hatukuharibu chochote. Tuliingia tu kwa ishara na kuondoka baada ya dakika 10.”

Kwa upande wao, viongozi wa msikiti wamelitaja tukio hilo kuwa ni kitendo cha uharibifu na uchokozi, siyo tu “kutii mrengo wa kisiasa” kama wanavyodai wahusika.

Generation Identity ni moja ya makundi yenye misimamo mikali ya wazungu wabaguzi barani Ulaya. Linajulikana kwa chuki dhidi ya wahamiaji na kupinga utamaduni wa mchanganyiko, na linapigia debe kile linachokiita kutimuliwa wahamiaji wasiokuwa wazungu. Kundi hili limepigwa marufuku nchini Ufaransa, na nembo yake (herufi ya Kigiriki "lambda") imepigwa marufuku Austria.

Msikiti wa Imam Ali (AS) Jijini Copenhagen

Mnamo mwaka 1994, kwa kuunganishwa kwa Kituo cha Al-Mustafa, Shule ya Lebanon, na Msikiti wa Muhammadiyah, hatua za mwanzo za kuanzisha msikiti mkubwa zaidi wa Kishia barani Ulaya zilichukuliwa.

Mnamo 2001, kwa juhudi kubwa za Hujjat-ul-Islam Sayyid Mohammad Mahdi Khademi, mwana wa Ayatullah Sayyid Hussein Khademi Isfahani, pamoja na msaada wa Marjaa wakubwa wa kidini, Taasisi ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS) na waumini, ardhi yenye ukubwa wa mita 3,000 ilinunuliwa kwa ajili ya kujenga msikiti wa kwanza wa Kishia katika moyo wa jiji la Copenhagen.

Hadi mwaka 2011, kituo hicho kikubwa cha Kiislamu kilikuwa kikitoa huduma zote muhimu kwa Mashia wa mataifa mbalimbali waliokuwa wakizungumza lugha tofauti kama vile Kidenmarki, Kiingereza, Kiarabu, Kiajemi, na Kiurdu.

Mnamo Septemba 2011, Waislamu wa Kishia walitaka kuibadilisha jengo la zamani kuwa msikiti wenye usanifu sahihi wa Kiislamu. Hatua hiyo ilihitaji kibali rasmi kutoka halmashauri ya jiji.

Siku ya kikao cha kutoa kibali katika ukumbi wa halmashauri ya jiji, umati mkubwa ulikusanyika nje, wakingoja uamuzi. Ghafla, sauti ya Allahu Akbar ilisikika kwa nguvu kutoka kwa watu, ikiashiria kuwa ujenzi wa msikiti huo umeidhinishwa. Machozi na tabasamu ya siku hiyo tukufu hayatasahaulika katika nyoyo za Waislamu wa Denmark.

Ujenzi wa msikiti ulianza rasmi mwaka huohuo, na msikiti ulifunguliwa rasmi katika siku tukufu ya Eid al-Ghadir mwaka 2015.

3493946

captcha