IQNA

Waziri Mkuu wa Denmark

Kupiga Marufuku uchomaji wa Qur’ani hakuzuii uhuru wa kujieleza

19:08 - August 04, 2023
Habari ID: 3477379
COPENHAGEN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Denmark amesema kupigwa marufuku kwa vitendo vya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu hakuwezi kuzuia uhuru wa kujieleza.

Katika mahojiano na gazeti la kila wiki la Denmark la Weekendavisen siku ya Alkhamisi, Mette Frederiksen alizungumzia wimbi la hivi karibuni la kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark, akibainisha kwamba kupigwa marufuku matukio hayo maovu hakutazuia uhuru wa kujieleza katika nchi hiyo.

Matamshi hayo yanakuja wakati watu wenye chuki dhidi ya Uislamu, hususan katika nchi za kaskazini mwa Ulaya na ukanda wa Nordic, wamekuwa wakitekeleza uchomaji moto wa mara kwa mara wa nakala za Qur'ani Tukufu, na vitendo vingine vya kuvunjia heshima Uislamu na Waislamu, katika wiki chache zilizopita.

Kundi la watu wenye msimamo mkali linalojiita Danske Patrioter (Wazalendo wa Denmark) limekuwa likivunjia heshima Qur’ani Tukufu mjini Copenhagen kwa siku kadhaa, likichoma nakala za kitabu hicho kitakatifu mbele ya balozi mbalimbali huku likitoa kauli mbiu zinazopinga Uislamu. Serikali ya Denmark imeeleza kushutumu vitendo hivi na imesema kwamba itachunguza uwezekano wa kuingilia kati wakati nchi, tamaduni na dini nyingine zinapolengwa ili kulinda usalama wa taifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmar Lars Lokke Rasmussen naye aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) kwamba nchi yake inalaani uchomaji moto wa Qur'ani na kueleza dhamira ya serikali ya kuingilia kati katika kesi maalum ndani ya mfumo wa uhuru wa kujieleza wa Denmark.

Hata hivyo, vyama vya upinzani nchini Denmark vinavyojumuisha vyama saba vimetoa pingamizi lao dhidi ya pendekezo la serikali la kukabiliana na uchomaji moto wa Qur'ani. Wamedai kuwa vitendo kama hivyo vinaweza kukaribisha uingiliaji wa kigeni katika siasa za Denmark na kudhoofisha uhuru wa raia.

3484628

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu denmark
captcha