IQNA

Iran yawasilisha malalamiko Denmark na Uswidi kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

11:12 - August 21, 2023
Habari ID: 3477471
TEHRAN (IQNA)- Iran imewaita wanadiplomasia wa Uswidi na Denmark katika mji mkuu Tehran kubainisha malalmiko yake makali kuhusu vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hizo mbili za Nordic.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Haki za Kibinadamu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliwaita maafisa hao wawili nyakati tofauti siku ya Jumapili.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amelaani vikali kuendelea vitendo viovu na vya kikatili vya kukitusi kitabu kitakatifu cha Waislamu katika nchi hizo mbili na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa serikali za Uswidi na Denmark zinapaswa kubeba dhima kamili na matokeo mabaya ya vitendo hivyo viovu.

Afisa huyo ametahadharisha zaidi juu ya kuendelea vitendo hivyo ambavyo amevitaja kuwa njama hatari huku akiashiria kauli ya hapo awali iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba kuwaunga mkono wahalifu na wanaoitukana Qur'ani Tukufu ni aina ya kutangaza vita dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.

Pia amewataka wanadiplomasia hao wawili kuzingatia wajibu wa kimataifa kulingana na Ibara ya 19 na 20 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), akisisitiza kuwa kanuni ya uhuru wa kujieleza inafungamana na wajibu na wajibu mahususi.

Afisa huyo amemaliza mazungumzo yake kwa kusema kuwa licha ya msimamo wa wazi na azma kubwa ya wanazuoni wapenda uhuru duniani katika kulaani kitendo hicho cha kufuru, lakini nchi za Uswidi na Denmark zimeendelea kutojali kufuata maazimio yaliyoidhinishwa na Baraza la Haki za Binadamu na vilevile Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusu suala hili.

Kwa upande wao wanadiplomasia hao wawili wamekumbushia misimamo ya nchi zao katika kulaani kitendo chochote cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kusema kuwa, serikali zao zimeazimia kuzuia vitendo hivyo kwa kufanya mabadiliko katika sheria zao za ndani.

Pia wamesema kuwa wataziarifu serikali zao kuhusu malalmiko ya Iran kuhusiana na vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Qur'ani Tukufu imekabiliwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima na watu wenye itikadi kali katika matukio matatu tofauti nchini Uswidi na Denmark, ambapo serikali za nchi hizo zimeidhinisha na kuhalalisha vitendo hivyo viovu kuwa ni "uhuru wa kujieleza."

Kashfa hiyo imechochea hasira ya Waislamu duniani kote. Nchi kadhaa zimewaita au kuwafukuza mabalozi wa Uswidi na Denmark.

3484858

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi denmark
captcha