IQNA

17:54 - February 24, 2021
Habari ID: 3473680
TEHRAN (IQNA)- Tarehe 13 Rajab mwaka wa 30 Amul Fil, kulitokea tukio kubwa na la kushangaza ambalo lilikuwa halijawahi kutokea na halitatokea tena katika historia ya mwanadamu. Hii ilikuwa tarehe ya kuzaliwa Imam Ali AS katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa wapenda uhuru na Waislamu duniani kote kwa mnasaba huu wa furaha wa kuzaliwa Ali bin Abi Talib AS ambaye ni jua la uadilifu wa wanadamu, mwana wa ami ya Mtume SAW, mkwewe, wasii na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake SAW.

Kama tulivyotangulia kusema, Imam Ali AS alikuwa mwana wa Abu Talib ambaye naye alikuwa mtoto wa Abdul Muttalib bin Hashim bin Abdul Manaf. Abu Talib alikuwa ami yake Mtume SAW na mama yake Imam Ali alikuwa Fatima bint Asad bin Abdul Manaf. Hivyo Imam Ali AS alikuwa kutoka ukoo wa Hashim katika pande zote mbili. Muhammad Maliki anasema hivi kuhusiana na kuzaliwa Imam Ali AS katika Nyumba ya al-Kaaba: 'Ali alizaliwa ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu katika mji wa Makka katika siku ya Ijumaa tarehe 13 mwezi wa Mwenyezi Mungu, Rajab mwaka wa 30 Amul Fil...... Kabla yake hakuna mtu mwingine aliyewahi kuzaliwa ndani ya nyumba hiyo na uzawa huo ilikuwa fadhila kubwa ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtunukia Ali AS kwa ajili ya kumtukuza na kunyanyua nafasi yake pamoja na kudhihirisha utukufu na heshima yake.' Hakim Neishaburi pia anasema: 'Kuzaliwa Ali ndani ya Kaaba ni jambo lililotufikia kupitia mapokezi mengi ya kuaminika. Hakuna mtu mwingine aliyewahi kupata fadhila hii hadi sasa.'

Kuzaliwa ndani ya al-Kaaba

Nafsi ya kitendo cha mtu kuzaliwa ndani ya al-Kaba tena kwa namna ambayo kuta zake zilipasuka na Fatima bint  Asad kupata fursa ya kuingia humo na kisha kutoka nje akiwa amembeba mikononi (kifuani) mtoto mchanga, chenyewe kinabainisha utukufu na fadhila za mtu huyo. Baadaye Imam Ali mwenyewe AS alikuja kuthibitisha utukufu na fadhila hizo kupitia matendo na mienendo yake ya maisha. Ali AS anatajwa kuwa muujiza hai wa malezi ya Mtukufu Mtume SAW. Hii ni kutokana na kuwa Imam Ali AS alitoa muhanga maisha yake kwa ajili ya kumlinda Mtume SAW na alikuwa ndugu na wasii wake. Mtume wa Rehema SAW anamtaja kuwa lango la elimu na maarifa yake kwa kusema: 'Mimi ni mji wa elimu na Ali ni lango lake, basi mtu anayetafuta elimu na apitie kwenye lango hilo.' Mtume SAW anasema katika sehemu nyingine: ' Mimi ni nyumba ya hekima na Ali ni mlango wake.'

Kwa hakika shakhsia ya Imam AS ni mkusanyiko wa mambo na sifa ambazo kila mojawapo ina uwezo wa kumfikisha mwanadamu katika kilele cha ukamilifu. Ukweli kwamba Imam Ali AS alikuwa mbora wa waja wa Mwenyezi Mungu katika kumuabudu umetejwa kuwa kipimo chake bora zaidi cha umaanawi. Alikuwa akisikiliza kwa makini  na kudiriki vyema minong'ono na dua za Mtume SAW alizokuwa akiziomba katika faragha na kufarijika nazo. Hii ndio maana akawa miongoni mwa watu wa kwanza kuukubali Uislamu na tokea hapo taratibu akawa na hamu kubwa ya kumwabudu Mwenyezi Mungu. Alikuwa akichukua hatua moja baada ya nyingine kuelekea kwa Mungu Muumba na kumwabudu kwa njia iliyostahiki. Kama yalivyo mawimbi kwenye bahari, Ali AS alizama kwenye utafutaji hakika na harakati pamoja na utulivu wake wote ulitokana na ukweli huo wa kutafuta haki. Hali ilikuwa kwa kiwango ambacho Mtume Mtukufu SAW alikuwa akiwaambia wapinzani wake: 'Msimlaumu Ali kwa sababu amezama kwenye dhati ya Mwenyezi Mungu.'

Subira ya Imam Ali AS

Kuhusu suala la kufanya subira na kusamehe, Imam Ali AS aliwashinda watu wote katika sifa hiyo ya kuvutia. Kiwango cha juu cha huruma yake kinaweza kuonekana wazi katika Vita vya Jamal na katika kuamiliana kwake na maadui na hasa Marwan bin Hakam na Abdallah bin Zubeir. Licha ya kuwa Imam Ali AS alikuwa amewashinda vitani na kuwadhibiti kikamilifu lakini aliwasamehe. Kamwe Imam Ali hakuwaadhibu wala kuwakandamiza wale walioshiriki katika vita hivyo vya Jamal wala watu wa Basra. Mnadi wake alikuwa akipaza sauti mjini kwa kusema: 'Kila mtu aliyekimbia medani ya vita hatafuatwa (hataandamwa). Hatuna tatizo na majeruhi, hakuna mateka atakayeuawa na mtu atakayeweka chini silaha yake atakuwa katika amani.' Ni wazi kuwa Imam Ali AS hapa alifuata kikamilifu mfano wa Mtume Mtukufu SAW katika ukombozi wa mji mtakatifu wa Makka kutoka mikononi mwa makafiri na mushrikina. Katika Vita vya Swiffin ni wazi kuwa ni watu wa Sham ndio walianza kumfungia yeye na wafuasi wake njia ya kufikia maji. Lakini Imam na wafuasi wake walipopata udhibiti wa vita hivyo, Imam AS aliulizwa: 'Je, tulizuie kufikia maji jeshi la Sham kama lilivyotufanyia sisi? Imam alijibu: 'Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, kamwe hatutafanya kama walivyofanya wao.'

Uhuru kwa mtazamo wa Imam Ali AS

Katika mantiki ya Imam Ali AS uhuru ni sehemu ya maumbile na fitra ya mwanadamu ambao unapaswa kuheshimiwa na kulindwa. Katika kipidi cha uongozi wa Imam Ali AS wapinzani walipewa uhuru mkubwa wa kudhihirisha imani na itikadi zao naye Imam na wafuasi wake wakipata fursa ya kukabiliana na itikadi potovu na za hadaa za wapinzani hao kwa kuwatolea hoja zenye nguvu. Maadui walikuwa wakifika msikitini na kuvuruga hotuba za Imam Ali AS Siku moja mtu alifika msikitini na kumuuliza swali Imam Ali ambaye alikuwa akihutubu kwenye mimbar. Imam AS alimjibu bila kusita. Hapo mmoja wa Makhawarij akapaza sauti na kusema: 'Mwenyezi Mungu amuue, ana elimu iliyoje!' Watu waliokuwa hapo walitaka kukabiliana naye lakini Imam akawakataza kwa hoja kwamba alimlenga yeye tu na sio watu wengine. Makhawarij hawakuwa wakiswali nyuma ya Imam Ali AS katika swala za jamaa kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuwa ni kafiri. Hivyo walikuwa wakifika msikitini lakini hawakuwa wakiswali nyuma yake bali walikuwa hata wakimuudhi kama tulivyoona hivi punde. Baada ya kuaga dunia Othman, baadhi ya watu walimwendea Imam ili kumbai. Imam aliwaambia wenyewe walipasa kuchukua uamuzi. Alisema: 'Suala la serikali ni katika masuala yenu na ni haki yenu kumchagua kiongozi mnayemtaka na wala hakuna mtu aliye na ruhusa ya kukutwisheni kiongozi.'

Uadilifu wa Imam Ali AS

Uadilifu ni sifa nyingine ya kuvutia iliyobainisha shakhsia ya Amir al-Mu'mineen Ali AS. Kama Imam angetaka kupuuza uadilifu na kufadhilisha mali ya dunia juu ya shakhsia yake bila shaka angekuwa khalifa aliyefanikiwa na mwenye nguvu zaidi katika zama zake. Lakini alikuwa amezama kwenye uadilifu, haki na kufanya usawa miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba ndugu yake mwenyewe Aqil alipomuomba ampe kiasi kidogo cha fedha kutoka Beitul Mal alichoma moto mikono yake ili kumtahadharisha na adhabu kali ya Siku ya Kiama. Uadilifu na usawa wa Imam Ali AS ni bendera inayopepea na kipimo cha uadilifu wa Uislamu. Imam anasema katika mafundisho yake kwamba: 'Mwenyezi Mungu alijaalia uadilifu kuwa msingi wa jamii ya mwanadamu.' Uislamu ni mwanga wa taa ya Uislamu na Uislamu usio na uadilifu ni mfano wa taa isiyoangaza.

Daima Imam Ali AS alikuwa akitembea katika njia ya marekebisho ya Umma wa Kiislamu. Hata kama watu walikosea katika kumchagua kiongozi wao mara tu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu SAW lakini hilo halikumfanya Imam achukue hatua za pupa na chuki katika kukabiliana na hali hiyo bali alifanya subira kubwa.

Hakuruhusu dunia imtawale

Kizuizi kikuu cha usalama  wa mwili na roho ya mwanadamu ni kuiabudu dunia. Imam Ali AS akiwa kiongozi wa jamii ya Kiislamu, licha ya kuwa alikuwa na vyanzo vyote vya utajiri  wa ardhi kubwa ya Waislamu, lakini hakuruhusu dunia na mapambo yake yamtawale. Alikuwa akisema: 'Ewe dunia! Nenda ukawahadae watu wengine wasiokuwa mimi, kwa sababu mkono wako hauwafikii watu kama Amir al-Mu'mineen.'

Msimamo na mwenendo wa Imam Ali AS kupuuza mvuto, mapambo na anasa za dunia, ulikuwa wa kuvutia kiasi kwamba alikuwa akifanya kazi mwenyewe katika mashamba ya mitende na kuichukulia kazi kuwa sehemu ya majukumu yake, ilihali mapato na mazao yaliyopatikana humo yalitumika kustawisha ardhi na mahitaji ya watu wengine. Kuhusu nafasi ya juu na fadhila tofauti muhimu za Imam Ali AS , Mtume SAW anasema kumuhusu Imam: 'Kila anayetaka kumtazama (kumfahamu/kumdiriki) Nabii Adam na elimu yake, Nuh na takwa yake, Ibrahim na subira yake, Musa na hofu yake na Isa na ibada yake basi na amtazame Ali bin Abi Talib.'

Kishikizo: imam ali as ، rajab
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: