
Hafla hii imehudhuriwa na kundi la maqari wahifadhi wa Qur'ani Tukufu kutoka Iran na Iraq, kwa lengo la kuenzi maneno ya Mwenyezi Mungu na kuimarisha udugu wa Kiislamu kupitia Qur’ani Tukufu
Kwa mujibu wa taarifa ya IQNA kutoka Qom, tarehe 27 Rajab ilitangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu mnamo mwaka 1389 Hijria Shamsia (sawa na 2010 Miladia) na uongozi wa Haram ya Imam Hussein (AS) nchini Iraq.
Siku ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu, ambayo ni miongoni mwa shughuli muhimu za Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu, huadhimishwa kila mwaka sambamba tarehe 27 Rajab. Kwa Waislamu, siku hii ina uzito wa pekee, kwani ndiyo siku ya Bi’tha, yaani kutumwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), na pia siku ambayo aya za mwanzo za Qur’ani Tukufu ziliteremshwa, na hivyo kufungua ukurasa mpya katika historia ya mwanadamu.
Sherehe hii ilianza kwa tilawa yenye kutuliza nyoyo ya Karim Mansuri, qari mashuhuri wa kimataifa wa Qur’ani Tukufu.
Kuitwa kwa Kongamano la Pili la Siku ya Kimataifa ya Qur’ani kwa jina la Abdulbasit
Pindi inapotajwa Qur’ani Tukufu, jina la Ustadh Abdulbasit Abdussamad hujitokeza mara moja katika fikra za wengi. Kwa heshima hiyo, kongamano hili lilianza kwa kukumbusha urithi na kumbukumbu ya qari huyu mkubwa, sambamba na kusomwa kwa Fat-ha kwa ajili ya roho yake. Kwa kufanya hivyo, waandaaji walitimiza wajibu wao kwa mmoja wa wenye sauti tamu zaidi katika historia ya tilawa ya Qur’ani, na hivyo kongamano hili la pili likapewa jina la Abdulbasit.

Baada ya kuoneshwa kipande cha video kilichoeleza wasifu na shughuli za Qur’ani za Ustadh Abdulbasit, Sayyid Muhammad Bahrul‑Ulum, Naibu Katibu Mkuu wa Haram ya Imam Hussein (AS) alitoa hotuba yake kwa lugha ya Kiarabu.
Kisha Mahdi Daghaghleh, qari wa kimataifa wa Qur’ani Tukufu, aliteka nyoyo za hadhira kwa kasida za kumsifu Mtume Muhammad (SAW) na Qur’ani. Katika sehemu nyingine ya kongamano hili, Hassan al‑Mansuri, mshauri wa masuala ya Qur’ani katika Haram ya Imam Hussein (AS), naye alitoa hotuba yake kwa lugha ya Kiarabu.
Njia ya kuokoka kutoka ukoloni mamboleo ni mageuzi ya sayansi ya jamii kwa mwanga wa Qur’ani
Katika mwendelezo wa mkusanyiko huu wa kiroho, Hujjatul‑Islam wal‑Muslimin Rezaei‑Esfahani, mfasiri wa Qur’ani Tukufu na mhadhiri mwandamizi wa Jami‘at al‑Mustafa al‑‘Alamiyya, alitoa pongezi zake kwa mnasaba wa sikukuu za mwezi wa Rajab na Siku ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu. Akizungumza kwa mtiririko wa kielimu, alieleza:
“Lau tungeuIliza Qur’ani Tukufu: Kwa wewe ni ujumbe ulimwengu wote? Katika sura mbalimbali, Qur’ani yenyewe inajibu kwa kauli yake tukufu: ‘Na hakika huu ni ukumbusho kwa walimwengu’ (Surat al‑An‘am, Aya ya 90).”
Hoja za Kinasaba na Kiakili Kuhusu Qur’ani kuwa ya ulimwengu mzima
Akizungumzia hoja za kinasaba (dalili za riwaya) zinazoonyesha kuwa Qur’ani Tukufu ni ya ulimwengu mzima, alieleza kuwa katika riwaya nyingi jambo hili limeangaziwa kwa uwazi. Miongoni mwa hizo ni hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imam Ridha (a.s.) inayobainisha kuwa Qur’ani Tukufu haikuteremshwa kwa ajili ya kipindi fulani tu. Ndiyo maana, kila tunapoisoma, hatuchoki wala hatuhisi kuchoshwa nayo; siri ya Qur’ani iko katika kudumu kwake milele. Kwa hivyo, haikuteremshwa kwa ajili ya kundi moja la watu, bali ni kwa ajili ya wanadamu wote duniani.
Rezaei‑Esfahani, akiendelea kubainisha kuwa mbali na hoja za kinasaba, kuna pia hoja ya kiakili kuhusu Qur’ani kuwa ya ulimwengu , alisema: Hoja ya kiakili ni kwamba ikiwa Qur’ani ndiyo kitabu cha mwisho cha mbinguni , na hakika ndivyo ilivyo , na ikiwa wanadamu katika zama zote na maeneo yote wanahitaji mwongozo wa Qur’ani, basi natija yake ni kwamba Qur’ani lazima iwe katika upatikanaji wa watu wote duniani.
Mikakati ya Kuitangaza na Kuieneza Qur’ani katika Ulimwengu
Akizungumzia mikakati ya kuufanya mwongozo wa Qur’ani uwe wa kimataifa, alibainisha kuwa njia hizo zimegawanywa katika makundi matatu: za utafiti, za kielimu, na za kiutendaji katika ulinganiaji na uenezi. Alisema kuwa mikakati ya kiutendaji na ya kimtandao katika kuieneza Qur’ani Tukufu inajumuisha kukuza mijadala ya kifonolojia na ya maneno ya Qur’ani, kuimarisha usomaji, uhifadhi na vikao vya tilawa, pamoja na kuhamasisha ulinganiaji unaozingatia maana na mafundisho ya Qur’ani.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupanua tafsiri na tarjuma za Qur’ani kwa lugha mbalimbali, kuanzisha na kuimarisha vituo vya Qur’ani na Darul‑Qur’ani, na kuandaa mashindano ya kitaifa na kimataifa ya Qur’ani Tukufu. Aliongeza kuwa taasisi na vyuo vya Qur’ani vinapaswa kuongeza juhudi katika uenezi wa mafundisho ya Qur’ani, sambamba na kukuza sanaa za Qur’ani kama khatt, nashid na kazi za kiutamaduni. Hatimaye, alitaja kuimarisha mitandao, majarida, vitabu na vyombo vya habari vya Qur’ani kuwa ni sehemu muhimu ya safari ya kuifikisha Qur’ani kwa jamii za ulimwengu kwa namna pana na yenye athari.
Kukabiliana na Ukoloni Mamboleo
Katika kuzungumzia njia ya kuokoka kutoka katika ukoloni mamboleo, mhadhiri mwandamizi wa Jami‘at al‑Mustafa al‑‘Alamiyya alieleza kuwa suluhisho la kweli linapatikana katika mageuzi ya sayansi ya jamii, na kwamba njia bora zaidi ya kuyabadilisha na kuyatengeneza upya masomo ya kibinadamu hupitia katika mwanga wa Qur’ani Tukufu.
Alisisitiza kuwa katika dunia ya leo, kuna haja kubwa ya kueneza mafundisho ya Uislamu halisi wenye misingi ya Ahul Bayt wa Mtume (SAW) kwa lugha mbalimbali ili kuyafikisha kwa watu wa mataifa tofauti.
Akiendelea na maelezo yake, alitaka Waislamu kutozuilia elimu ya Qur’ani na mafundisho ya Ahlul‑Bayt wa Mtume (SAW) ndani ya mipaka ya nchi yao pekee, bali kuyafikisha kwa ulimwengu mzima. Alisema kuwa ni muhimu kuachana na utamaduni wa kufanya kazi kwa mtindo wa visiwa visivyo na mawasiliano. Leo, miji muhimu ya Kiislamu kama Qom, Najaf na Mashhad, pamoja na vituo mbalimbali vya Qur’ani, vimefanya kazi kubwa na ya thamani; hata hivyo, bado hakuna nguvu ya pamoja inayounganisha juhudi hizi ili kutoa matokeo makubwa zaidi kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Katika hafla hii, Hujjatul‑Islam wal‑Muslimin Rezaei‑Esfahani, Sayyid Muhammad Bahrul‑Ulum na Riyadh al‑Hakim, miongoni mwa watendaji na wahudumu wa Qur’ani, walituzwa na kuheshimiwa kwa mchango wao katika kueneza elimu na nuru ya Qur’ani Tukufu. Vilevile, shukrani maalumu zilitolewa kwa Haram ya Hadhra Abbas (AS) kwa juhudi zao katika kuandaa na kuendesha kongamano hili kwa umakini na heshima kubwa.
Katika maazimio ya Kongamano la Pili la Siku ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu, ilikubaliwa kwamba, kwa niaba ya marehemu Sheikh Abdulbasit Abdussamad, qari mashuhuri na mwenye athari kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, mtoto wake atapewa heshima maalumu kama ishara ya kutambua nafasi ya baba yake katika historia ya tilawa ya Qur’ani.
4328047