Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika ujumbe wake katika maadhimisho ya "Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina" kuwa: Kila mwaka katika siku kama hii jamii ya kimataifa inasimama na kudhihirisha mshikamano wake ili kulinda utu, haki, uadilifu na haki ya wananchi wa Palestina ya kujiainishia mustakbali wao. Tarehe 29 Novemba kila mwaka hukumbusha matukio machungu yaliyojiri huko nyuma ikiwemo kuwasilishwa azimio lisilo la haki la kuigawa Palestina. Siku hii pia ni siku ya kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina, na ni siku ambayo Palestina ilichaguliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa
Tarehe 29 Novemba 1947 Baraza Kuu la UN lilipasisha azimio lisilo la kiadilifu kwa lengo la kuigawa Palestina na kisha kulitambua rasmi. Kwa mujibu wa azimio nambari 181; Palestina iligawanywa katika sehemu mbili, na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likazingatia sehemu moja ya ardhi ya Palestina kuwa kwa ajili ya kuasisi utawala wa Kizayuni na nyingine kwa ajili ya kuunda nchi na serikali ya Palestina. Ingawa azimio hilo lisilo la kiadilifu la kuigawa Palestina lilipuuza kuwa ardhi ya Palestina ni milki ya Palestina karibu nusu yake ilizingatiwa kwa ajili ya kupatiwa Wapalestina na nusu nyingine kwa ajili ya Wazayuni. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 1948 Wazayuni hawakuvumilia pia hata kutolewa nusu ya ardhi ya Palestina kwa wakazi wake wa asili, bali walizikalia kwa mabavu ardhi hizo ambapo hadi leo wamekuwa kikwazo cha kuundwa nchi huru ya Palestina.Takwimu kutoka Gaza zinaonyesha kujiri jinai za kutisha; watu waliouawa shahidi, majeruhi wengi wakiwemo wale waliokatwa viungo vya mwili, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu waliouawa kwa umati na majengo yaliyobomolewa vitani na hivyo kudhihirisha ukubwa wa maafa katika eneo hilo lililozingirwa. Wakati huo huo kumetolewa ripoti nyingi za kutisha kuhusu jinai za karibuni katika Ukingo wa Magharibi. Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa tangu kuanza mashambulizi na vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza Oktoba 7 mwaka jana hadi sasa watu elfu 44 wameuliwa shahidi na wengine 104,933 kujeruhiwa.
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe akiwahutubu viongozi na wakuu wa mataifa mbalimbali kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina kwamba: Tarehe 29 Novemba ni Siku ya Kimataifa ya Mshikamano, ni siku ya mshikamano wa dunia na ujasiri na mapambano, ni siku ya wananchi kupigania uhuru na ukombozi ambapo wamesimama kidete na kuendesha mapambano kwa mikono mitupu kwa zaidi ya miongo saba dhidi wanajeshi katili zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu. Jeshi ambalo hujifakharisha kwa kuua watoto wachanga, kuua watu wasio na ulinzi, kuharibu nyumba za watu na kuua mashujaa wakubwa bila woga wala haya mbele ya macho ya walimwengu.
Kuwanusuru wananchi wa Palestina
Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia umeeleza kuwa: Hali ya leo ya Palestina na nchi nyingine zilizoathiriwa na mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel inathibitisha kuwa hatua madhubuti na za haraka zaidi za kuwasaidia na kuwanusuru wananchi wa Palestina ni kuudhibiti utawala wa Kizayuni na kusitisha misaada na uungaji mkono wa kimataifa kwa donda hilo la saratani. Utawala wa Kizayuni umethibitisha kutozingatia wala kuheshimu kanuni na maadili ya kimataifa kwa kuchana hadharani Hati ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni marejeo yanayokubalika na nchi wanachama wa umoja huo.
Historia itasajili kutekelezwa mauaji makubwa ya kimbari dhidi ya raia, mashambulzi dhidi ya hospitali, kukatwaa huduma ya maji kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza, kuzuiwa misaada ya chakula, mafuta na dawa kuwafikia raia hao, kuwafanya wakimbizi maelfu ya watu, mauaji dhidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa taasisi za kimataifa na kuuawa shakhsia watajika kama mashahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Ismail Haniyeh na shahidi Yahya Sinwar kwa kushirikiana na serikali za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu khususan Marekani; ambapo mara zote jitihada za kusitisha vita na mauaji ya watoto ziliambulia patupu kwa kuinuliwa juu mkono wa upinzani wa Mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
/4251200