
Naye Omran al Zoubi Waziri wa Habari wa Syria amesema makubaliano hayo ya kihistoria ni ushindi wa kutumiwa mantiki ya mazungumzo na njia za kisiasa dhidi ya vitisho, changamoto na vita. Kuwaiti pia imekaribisha makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi 5 wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Iraq, Uturuki, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan pia zimetangaza kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Wakati huo huo Ufaransa imesema kuwa, kuna uwezekano mwezi Disemba Umoja wa Ulaya ukaiondolea Iran baadhi ya vikwazo kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na nchi za Magharibi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon pia ametoa tamko na kupongeza makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na madola matano yenye nguvu duniani na kuyataja kuwa ya kihistoria
Baada ya kupita siku kadhaa za mazungumzo hayo huko Geneva hatimaye siku ya Jumapili ya tarehe 24 Novemba kulifikiwa hatua ya kutiwa saini makubaliano ya awali ambayo miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani ilitambuliwa rasmi na nchi zinazounda kundi la 5+1. Kufuatia kutiwa saini makubaliano hayo, Rais Hassan Rouhani alisema kuwa, taifa la Iran halikuwa na halitakuwa na nia kabisa ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia.
Wakati huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameisifu timu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoshiriki kwenye mazungumzo ya nyuklia na kundi la 5+1 kwa jitihada zake kwenye uwanja huo. Kiongozi Muadhamu ametoa pongezi hizo wakati alipojibu barua aliyoandikiwa na Rais Hassan Rouhani kuhusu mazungumzo hayo.
1322492