Katika mji wa al-Khalil, walowezi hao walichoma moto nyumba mbili katika kijij cha al-Tuwani huko Masafer Yatta na kuteketeza msikiti wa eneo hilo, na kusababisha uharibifu mkubwa. Aidha, waliharibu mali nyingine, ikiwemo gari, huku wanajeshi wa Kizayuni wakitoa ulinzi wa moja kwa moja kwa wahalifu hao.
Katika eneo la Wadi al-Rakhim karibu na Yatta, walowezi walivamia nyumba mbili na kuiba kondoo watatu, wakati ambapo wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikuwa wakifyatua risasi za moto katika eneo hilo, ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa. Katika mji wa al-Samu, walowezi wenye silaha walijaribu kupora mifugo huko Wadi Ajhish lakini walilazimika kurudi nyuma baada ya kukabiliwa kishujaa na wakazi wa eneo hilo.
Katika mji wa Nablus, walowezi walishambulia eneo la al-Dhahr nje kidogo ya mji wa Beita, na kusababisha majeraha kwa Wapalestina wanne, huku wakiharibu nyumba na mali zao. Katika shambulizi jingine tofauti karibu na Burqa, kijana mmoja alijeruhiwa mkono. Jumamosi jioni, walowezi walichoma moto nyumba ya mkazi mmoja ambaye amekuwa akilengwa mara kwa mara; nyumba hiyo ilikuwa na watu ndani wakati wa shambulizi hilo na iliteketea kabisa.
Kwa mujibu wa Tume ya Palestina ya Kupinga Ukuta wa Kibaguzi na Ujenzi wa Vitongoji vya Kiyahudi , vikosi vya utawala ghasibu wa Israel na magenge ya walowezi wamefanya ukiukwaji wa haki za binadamu mara 11,074 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026. Hii ni pamoja na mashambulizi 3,488 ya walowezi yaliyohusisha uvamizi wa vijiji, mashambulizi dhidi ya raia, uchomaji moto, uporaji wa ardhi, na ujenzi wa vitongoji haramu. Mashambulizi haya ya kinyama yamesababisha mashahidi 17 miongoni mwa Wapalestina. Nablus ilirekodi idadi kubwa zaidi ya matukio hayo (900), ikifuatiwa na al-Khalil (840), na Ramallah–al-Bireh (780).
/3498334