Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA,Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha mauaji na umwagikaji damu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka Waislamu na Wakristo nchini humo washirikiane kwa minajili ya kuijenga nchi yao. Ban Ki moon ameitaka jamii ya kimataifa kushirikiana katika kupeleka misaada ya kibinadamu Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wakati huohuo, kundi la Anti Balaka limewashambulia na kuwaua Waislamu watatu waliokuwa ndani ya gari ndogo ya abiria kwa kuwapiga risasi na kuwakatakata kwa visu na mapanga karibu na uwanja wa ndege wa Bangui.
Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch lilitaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuzuia mauaji ya halaiki ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waislamu ni takribani asilimia 15 ya watu milioni 4.6 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ripoti zinasema kuwa magenge ya magaidi Wakristo wenye misimamo mikali wamewaua maelfu ya Waislamu nchini humo huku mamia ya maelfu wakilazimika kukimbilia katika nchi jirani. Kuna askari 1,600 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magaidi Wakristo.
1378500