Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Askofu Desmond Tutu ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ameongeza kuwa mwendelezo wa vitendo vya mauaji vinavyofanywa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka dhidi ya Waislamu nchini humo, ni jambo litakalosababisha nchi hiyo kutumbukia kwenye mauaji ya kimbari. Matamshi ya Askofu Tutu yanatolewa katika hali ambayo, ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR imeeleza kwamba, idadi kubwa ya Waislamu wa nchi hiyo wamelazimika kuwa wakimbizi baada ya kusakamwa na kushambuliwa na mashambulio ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka. Ripoti hiyo ya UNHCR imeongeza kuwa, idadi kubwa ya watoto wa Kiislamu inakabiliwa na tatizo la lishe duni. Duru za habari zinaeleza kuwa, kila wiki zaidi ya Waislamu elfu kumi wakiwemo wanawake na watoto hulazimika kuyakimbia makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa na wanamgambo hao.