IQNA

Ufahamu usiokuwa sahihi wa Wamagharibi kuhusu Uislamu ni matokeo ya propaganda chafu za vyombo vya habari

13:57 - November 02, 2008
Habari ID: 1703261
Wananchi wengi wa nchi za Magharibi huamiliana na Waislamu na kuchukua maamuzi yao kuhusu wafuasi wa dini hiyo kwa mujibu wa propaganda za kichochezi za vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Waislamu. Wananchi hao hutosheka na habari hizo zisizokuwa sahihi na huutambua Uislamu kupitia vyombo vya kichochezi vya Magharibi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Redio ya Arifan ya Uturuki Mehmet Emin Genc na kuongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa wimbi kubwa la kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu na Mtume Muhammad SAW jambo ambalo linatokana na uchache wa maarifa ya Wamagharibi kuhusu dini tukufu ya Kiislamu. Amesema kuwa katika nchi zisizokuwa za Kiislamu watu hutambua dini ya Kiislamu kupitia watu wengine na kuwa na ufahamu potofu wanaoupata kupitia wanafiki. Mehmet Emin Genc amesema, watu katika nchi zisizokuwa za Kiislamu hutoa maamuzi yao kuhusu Uislamu bila ya kutilia maanani mafundisho ya dini hiyo wala kitabu cha Qurani na kwamba inasikitisha kuona kuwa propaganda chafu dhidi ya Uislamu zimeshika kasi kwa kadiri kwamba ni vigumu kubadili maamuzi kama hayo.
Mkurugenzi wa Radio Arifan ya Uturuki ameashiria majukumu ya Waislamu katika uwanja huo na kusema kuwa ili kuweza kukabiliana na harakati za kuupiga vita Uislamu katika nchi za Magharibi hapana budi kubainisha Uislamu halisi na kutumia zana zote zinazowezekana kwa ajili ya kukabiliana na hujuma za kitamaduni za Wamagharibi.
Mkurugenzi wa Radio Arifan amesema kuwa lengo la kuanzishwa radio hiyo ni kujenga hisia za udugu kati ya Waislamu wa Uturuki na kwamba itikadi za madhehebu zote za Kiislamu zinazingatiwa katika kutayarisha vipindi vya radio hiyo. Amesema kuwa hii leo kuna njama za kuzusha mfarakano kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kwa kuvuruga utulivu na kihoro na mshikamano wa wafusi wa dini hiyo kote duniani.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Mehmet Emin Genc ameashiria matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Sheikh Yusuf Qardhawi mwanachuoni Mmisri anayeishi Qatar na akasema, matamshi yake yametokana na chuki za kimadhehebu zisizokuwa na msingi. Amesema, chuki za kimadhehebu haziwahusu watu majahili pekee bali wanazuoni na wasomi pia hukumbwa na tatizo hilo. 313556
captcha