IQNA

Kongamano la Wanawake Wafanyakazi Katika Nchi za Kiislamu Kufanyika nchini Syria

13:55 - November 02, 2008
Habari ID: 1703264
Kongamano la Wanawake Wafanyakazi Katika Nchi za Kiislamu chini ya anuani ya "Nafasi ya Utamaduni, Vyombo vya Habari na Utalii Katika Ustawi Endelevu" litaanza tarehe 2 hadi 4 za mwezi huu wa Novemba katika mji mkuu wa Syria, Damascus.
Mwandishi wetu wa Syria ameripoti kuwa kongamano hilo litafanyika kutokana na juhudi za kamati ya Wanawake Wafanyakazi wanachama wa Chumba cha Biashara cha Damascus kwa kushirikiana na Muungano wa Jumuiya za Biashara za Syria, Taasisi ya Kiislamu ya Viwanda na Biashara, Benki ya Ustawi ya Kiislamu na Mpango wa Ustawi wa Umoja wa Mataifa. Kongamano hilo limeitishwa kwa mnasaba wa kuteuliwa mji wa Damascus kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiarabu.
Kongamano hilo ambalo litahudhuriwa na zaidi ya shakhsia 150 kutoka nchi 40 wanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na jumuiya nyingine za kimataifa litabainisha nafasi muhimu ya wanawake wanaofanyakazi katika ustawi wa nchi za Kiislamu na kustawisha uhusiano wa kiuchumi kwa ajili ya kukabiliana na athari mbaya za utandawazi kupitia njia za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kiutamaduni, utalii na masuala ya kijamii.
Sambamba na kongamano hilo kutafanyika maonyesho ya dawa, vipodozi, utengenezaji wa vito, uchoraji na kadhalika ambavyo ni matokeo ya kazi za wanawake wanaofanya kazi katika nchi za Kiislamu wanachama katika jumuiya ya OIC. 313464
captcha