IQNA

Hadhi ya familia inapaswa kuzingatiwa katika sheria za kimataifa

10:41 - November 04, 2008
Habari ID: 1704316
Katika hali ya sasa familia katika nchi za Magharibi zinatumiwa kama chombo cha kutimizia maslahi ya kimaada, kwa msingi huo Jumuiya ya Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu inafanya jitihada za kuitisha mazungumzo kati ya dini mbalimbali ili kujadili suala la kuzingatiwa utukufu wa familia katika sheria za kimataifa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu ya Iran Mahdi Mustafawi katika kikao cha tatu cha kidini cha kituo cha mazungumzo kati ya dini mbalimbali na kanisa la Orthodox. Bwana Mustafawi ameongeza kuwa kuitishwa kwa vikao kama hivyo ni matokeo ya fikra za kupenda kuishi pamoja kwa amani, kusaidia na ushirikiano wa kidugu kati ya dini mbalimbali.
Amesema kuwa Mwenyezi Mungu amemtunuku mwanadamu neema ya mawasiliano ya kirafiki na kidugu na akaongeza kuwa anatarajia matumizi ya neema hiyo ya Mwenyezi Mungu ambayo inastawi zaidi kutokana na teknolojia ya kisasa yatakuwa kigezo bora kwa nchi nyingine.
Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Waislamu na wafuasi wa dini za wachache hapa nchini Iran katika nyanja za elimu na utafiti na akasema kuwa kuimarishwa ushirikiano kati ya dini mbalimbali kunapaswa kufanyika katika fremu ya mahitaji ya jamii. Ameashiria kwamba, kikao hicho kilijadili umuhimu wa nafasi ya familia katika dini mbalimbali na kuongeza kuwa familia kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu na Ukristo, ndiyo nguzo kuu ya jamii ambayo pia ina mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa mwanadamu. Amesema, ni kwa sababu hiyo ndiyo maana wanafikra wa dini za mwenyezi Mungu wakatoa kipaumbele maalumu kwa suala la kustawisha na kuboresha taasisi ya familia.
Mustafawi amesema, dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kusambaratika taasisi ya familia katika nchi mbalimbali. Amesema kuwa wasomi na wanazuoni wa kidini ndio wenye wadhifa wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Ameashiria juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuimarisha misingi ya taasisi ya familia na akasema, sheria za nchi hiyo zinatokana na kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu ambaye anajua maslahi halisi ya mwanadamu na kwamba kufuata sheria za kitabu hicho kunaweza kumfikisha mwanadamu katika lengo linalokusudiwa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Mahdi Mustafawi ameelezea kusikitishwa na ukweli kwamba, sheria za kimataifa zimebuniwa kwa kuzingatia fikra za kiseculari na kihumanism na akasema, katika kipindi cha sasa familia katika nchi za Magharibi zinatumiwa kwa shabaha ya kufikia maslahi ya kimaada na kwamba Iran inafanya jitihada za kusisitiza juu ya utukufu wa familia katika sheria za kimataifa. 315202
captcha