Kongamano la kimataifa lililochunguza sheria za kiutekelezaji, aya za Qurani na kanuni za Kiislamu kuhusu haki za wanawake wa Kiislamu limefanyika katika mji mkuu wa Yemen, San'aa.
Shirika rasmi la habari la Yemen SABA limeripoti kuwa kongamano hilo linasimamiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Yemen kwa kushirikiana na Kitengo cha Utamaduni cha Syria mjini San'aa. Wanafikra na wasomi kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu na Kiarabu wameshiriki katika kongamano hilo.
Al Qadhi Hussein al Mahdi ambaye ni mjumbe wa Mahakama Kuu ya Yemen amewasilisha makala katika kongamano hilo la kimataifa akichunguza haki za mwanamke katika sheria za Kiislamu na kusisitiza kwamba, dini hiyo tukufu inatilia mkazo suala la kulindwa hadhi na haki za kijamii na kiuchumi za wanawake. Hussein al Mahdi amesema, Uislamu umempa mwanamke haki ya uhuru wa kujieleza, kuchagua na kushiriki katika masuala mbalimbali.
Mtafiti wa Kiyemen Bibi Aala Talal al Tal amechunguza hali ya wanawake wa Kiarabu katika vipindi mbalimbali vya historia ikiwa ni pamoja na kipindi cha kabla ya Uislamu na kufafanua haki za wanawake katika Uislamu. Bibi Talal al Tal amewataka wanawake wa Kiislamu kuwa macho mbele ya hujuma za kipropaganda za nchi za Magharibi na matakwa yao yanayomhimiza mwanamke kuondoka katika nafasi yake ya asili na kupunguza mchango wake katika familia.
Kwa upande wake mtafiti wa Qatar Muhammad al Shaikhan amezungumzia haki za binadamu katika Uislamu akisema kuwa Wamagharibi wanafanya jitihada za kueneza ada na desturi zao zisizokuwa sahihi katika jamii za Kiislamu na kwamba kuna haja ya kuzima njama hizo kwa upashaji habari sahihi na kuwahimiza wanawake wa Kiislamu kurejea kwenye misingi ya sheria za Kiislamu. 318776