Ayatullah Fadhlullah ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu wa Kiislamu wa Ivory Coast Abubakr Fofana na akaongeza kuwa, suala la kuwepo umoja wa Kiislamu si hamu na takwa la kimoyo tu, bali ni nguzo muhimu ya kuendelea kuwepo Waislamu wenyewe. Amesema kuwa umoja kati ya Waislamu ndiyo nguzo muhimu ya kubakia hai wafuasi wa dini hiyo na amewahimiza Waislamu wote kufanya jitihada za kufafanua sura halisi ya Uislamu.
Allamah Fadhlullah ambaye ni marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini ameashiria mashinikizo yanayofanywa dhidi ya Waislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi sambamba na hujuma kubwa za kipropaganda dhidi ya dini ya Kiislamu na akasema, kuna udharura wa kukabiliana na hujuma hizo kwa kulinda umoja na mshikamano wa ndani na kutumia vyombo vya habari na kiutamaduni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu wa Kiislamu wa Ivory Coast ameeleza uzoefu wa baraza hilo katika harakati za Kiislamu barani Afrika na taathira mbaya ya hitilafu kati ya Waislamu. Amezungumzia pia umuhimu wa miradi ya kiutamaduni na kifikra nchini Ivory Coast. 321521