Chama cha Ukombozi wa Kiislamu cha Iraq kimetangaza kuwa kutiwa saini makubaliano ya kiusalama kati ya Baghdad na Washington ni sawa na kuhalalisha kukaliwa kwa mabavu adhi ya Iraq. Taarifa ya chama hicho imesema, hatua hiyo itakuwa ni kuiuza ardhi ya Iraq.
Kituo cha Quds Press kimeripoti kuwa taarifa ya chama cha Ukombozi wa Kiislamu cha Iraq imesema: Vipengee vya makubaliano hayo vinadhamini maslahi ya Marekani peke yake nchini Iraq. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Marekani inafuatilia maslahi makubwa ya kisiasa na kiuchumi kwa kutaka kutiwa saini makubaliano hayo ya kiusalama na inafanya juhudi za kudhibiti eneo la Mashariki ya Kati na utajiri wa Iraq ikiwa ni pamoja na mafuta ya nchi hiyo.
Taarifa ya chama cha Ukombozi wa Kiislamu cha Iraq imesisitiza kuwa Wairaqi wanaweza kuwashinda askari vamizi na kuwafukuza katika nchi yao na hatimaye kurejesha hadhi na heshima ya taifa lao.