IQNA

Waislamu wanapasa kukabiliana kimantiki na vitendo vya dharau dhidi ya matukufu yao

17:04 - November 29, 2008
Habari ID: 1713930
Waislamu hawapasi kukabiliana na dharau dhidi ya matukufu yao kwa njia zisizofaa, bali wanawajibika kutumia njia za kielimu na kimantiki katika kupambana na jambo hilo huku wakizingatia umoja na mshikamano kati yao.
Hayo yamesemwa na Omar Ihrishan, mwanachama wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Kiislamu na vilevile muhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdallah II cha mjini Rabat Morocco, katika mazungumzo yake na mwandishi wa Shirika la Habari za Qur’ani la Kimataifa IQNA. Amesema, udhaifu wa Waislamu katika kukabiliana na dharau pamoja na matusi yanayotolewa na maadui wa Uislamu dhidi ya matukufu ya Kiislamu umepelekea kutolewa kwa picha potofu na maadui hao ulimwenguni. Amesisitiza kwamba, Waislamu hawapasi kukabiliana na dharau kama hizo kwa kutoa nara tupu na zisizo na muelekeo kwa sababu jambo hilo linaudhuru Uislamu badala ya kuutetea. Amesisitiza kwamba, njia za kielimu na kimantiki zinapasa kufuatwa katika kukabiliana na matusi hayo dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu.
Bwana Ahrishan ameendelea kusema katika mahojiano yake na IQNA kwamba, kufanyika vikao kama cha hivi karibuni cha ‘fikra ya pamoja ya wanachuo wa ulimwengu wa Kiislamu’ kuna umuhimu mkubwa katika kuwaunganisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na hujuma ya nchi za Magharibi dhidi ya Waislamu na Uislamu. Amesema, wanachuo ndio muhimuli halisi wa kuleta umoja na shikamano katika jamii na kwa hivyo wana athari kubwa katika uwanja huo. Ahrishan amesema kuwa, kuna umuhimu na udharura mkubwa wa kuwepo umoja wa Waislamu katika ulimwengu wa sasa na kwamba, Waislamu wanapasa kuzingatia suala hilo la sivyo waangamie katika dimbwi la hitilafu zinazozushwa na maadui. Amesema, kusoma kwa bidii linapasa kuwa lengo kuu la wanachuo wa Kiislamu na kwamba wanapasa kufanya juhudi maradufu kwa ajili ya kuimarisha kiwango cha elimu na utafiti katika nchi zao. 327239
captcha