Mamia ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Qatif nchini Saudi Arabia wamefanya maandamano wakipinga mzingiro unaoendelea kufanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji hao waliokuwa na mabango yenye maandishi yanayolaani ukatili wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, walikemea vikali mzingiro wa utawala huo dhidi ya wakazi wa Gaza na uungaji mkono wa Marekani kwa mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo wa kibaguzi huko Palestina.
Waandamanaji hao ambao walibeba picha za Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah, walimpongeza pia mwandishi habari wa Iraq aliyemshambulia kwa viatu Rais George Bush wa Marekani. Vilevile wameitaka Misri kufungua kivuko cha Rafah na kuvunja mzingiro wa Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Wakazi milioni moja na nusu wa eneo hilo wanaishi katika hali ya kusikitisha kutokana na mzingiro huo za Israel ambayo imezuia kuingizwa mahitaji muhimu na ya kimsingi kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo. 336054