IQNA

Maulamaa Waislamu na Wakristo nchini Syria walaani jinai za Israel huko Gaza

9:06 - December 31, 2008
Habari ID: 1725267
Maulamaa Waislamu na Wakristo nchini Syria wametoa taarifa wakilaani jinai za Israel katika Ukanda Gaza.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Syria SANA, Maulamaa Waislamu na Wakristo nchini humo wametoa taarifa wakilaani kimya cha nchi za Kiarabu na njama za kimataifa katika mauaji, uharibifu na jinai nyinginezo zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko Gaza.
Taarifa hiyo imesema kuwa: “Kinachotokea hivi sasa huko Gaza ikiwa ni pamoja na mauaji ya watoto, wanawake na wazee pamoja na kuharibiwa shule, misikiti na vyuo vikuu ni mkasa mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia”.
Maulamaa wa Kiislamu aidha wametoa wito kwa maulamaa wanchi zote za Kiarabu na Kiislamu na jumuiya za kimataifa kutumia uwezo wao wote kuushinikiza utawala katili wa Israel usitishe jinai zake huko Gaza.
“Pamoja na njama zote za utawala ghasibu wa Israel zinazoandamana na mashambulizi makali ya kijeshi ya nchi kavu, angani na majini kwa lengo la kuangamiza Gaza, utawala huo hautapata chochote ghairi ya kufeli na taifa la Palestina halitasalmu amri bali hatimaye litapata uhuru, usalama na amani”, wamesema maulamaa hao.
Taarifa hiyo imeashiria misimamo ya Syria na kusema: “Syria inataka nchi za Kiarabu na Kiislamu kudumisha umoja na mshikamano na kutumia tadbiri inayohitajika kutafuta njia muafaka za kuzuia kukita mizizi utawala ghasibu wa Israel. Mojawapo ya hatua ndogo zaidi zinazoweza kuchukuliwa ni kukata uhusiano wote na utawala huo ghasibu na kuwafukuka mabalozi wake walioko katika miji mikuu ya nchi za Kiarabu na Kiislamu”, imesisitiza taarifa hiyo.
Wakati wa kusomwa taarifa hiyo Waziri wa Waqfu wa Syria Muhammad Abdulsattar as-Sayid, Mufti wa Syria Sheikh Badrudin Hasun na Askofu Luka al Huri walisisitiza kuwa: “Syria itaendelea kubeba mwenge wa mapambano,na adui Muisraeli hawezi kufikia malengo yake huko Gaza”.
Viongozi wa kanisa za Kikristo nchini Syria wametoa taarifa tofauti na kulaani vikali jinai za Israel huko Ghaza. Wamesisitiza kuwa historia haijawahi kushuhudia unyama unaotendwa na Israel hivi sasa huko Palestina.
Katika taarifa yao, viongozi hao wa Kikristo nchini Syria wametoa wito kwa jamii ya wanadamu duniani na hasa Waarabu, mashirika ya kidini na yale ya kutetea haki za binadamu pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kwa lengo la kuzuia mauji ya kimbari na mkasa wa kibinadamu huko Gaza. Wamesisitiza kuwa Israel ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria zote za kimataifa. Aidha wamesema, vitendo vya utawala haramu wa Israel vinaenda kinyume kabisa na mafunzo ya dini zote za mbinguni. 341101


captcha