Kundi la maulamaa na wanafikra wa Kiislamu limetoa taarifa ya pamoja likisema kuwa hatua ya serikali ya Misri ya kufunga kituo cha mpakani cha Rafah na ushirikiano wa baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel ni usaliti mkubwa zaidi kwa umma wa Kiislamu katika kipindi chote cha historia.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na zaidi ya wasomi mia moja wa Kiislamu kutoka pembe mbalimbali duniani imesema: Kufunga kivuko cha Rafah na kuzuia dawa, chakula na misaada mingine ya kibinadamu kwa watu wa Gaza ni kushirikiana moja kwa moja na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuwaua raia wa eneo hilo wakiwemo wanawake na watoto wasiokuwa na hatia.
Katika taarifa hiyo maulamaa wa Kiislamu wamewataka Mamufti na wanazuoni wa kidini kutoa fatuwa ya kwenda kupigana jihadi ili kuwanusuru raia wasiokuwa na hatia wa Ukanda wa Gaza na kufafanua misingi ya sheria za Kiislamu kuhusu suala la kuwahami watu wa Gaza.
Taarifa hiyo pia imezitaka jumuiya na vyombo vya ulinganiaji vya Kiislamu kuwasaidia wapiganaji wa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu huko Gaza na kuwaelimisha walimwengu kuhusu jinai zinazofanywa na Israel katika eneo hilo. 348227