Mfalme Muhammad VI aliyasema hayo katika mkutano wa Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu unaofanyika mjini Rabat. Amesema kuwa viongozi wa sekta ya mawasiliano wanawajibika kutumia vyema suhula za kisasa katika medani ya mawasiliano kwa lengo la kuweka wazi malengo na kuiarifisha jamii ya Kiislamu na misimamo halisi ya dini hiyo kwa walimwengu.
Amesema kuwa, kuna udharura mkubwa wa kutayarisha uwanja wa kuwepo mazungumzo ya dini na tamaduni nyinginezo katika dunia ya sasa na kwamba vyombo vya mawasiliano vya Kiislamu vinapaswa kulitilia maanani suala hilo.
Miongoni mwa maudhui zinazojadiliwa katika kikao cha sasa cha Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu ambacho kinafanyika sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 40 wa kuundwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), ni kadhia ya kustawisha Shirika la Habari la Kimataifa la Kiislamu (IINA) na Jumuiya ya Redio za Kiislamu (ISBU). 355664