IQNA

Kuanza kikao cha Mawaziri wa Masuala ya Watoto wa nchi za Kiislamu huko Sudan

8:47 - February 03, 2009
Habari ID: 1739327
Kikao cha pili cha kimataifa cha Mawaziri Wanaoshughulikia Masuala ya Watoto wa nchi za Kiislamu kimefunguliwa mjini Khartoum Sudan kwa kaulimbiu ya "Mustakbali wa Kung'ara kwa Ajili ya Watoto." Kikao hicho kinafanyika kwa hima ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (ISESCO) na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNISEF).
Washiriki katika kikao hicho ambacho kinasimamiwa na Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan watajadili na kubadilishana mawazo kuhusu mustakbali wa watoto katika ulimwengu wa Kiislamu na kadhia ya kuasisi kamati ya kuwalinda watoto wadogo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Washiriki katika kikao hicho wanajadili pia utafiti wa ISESCO kuhusu matatizo ya watoto katika nchi za Kiislamu, masuala ya afya na elimu na kadhia ya kuwalinda watoto na changamoto za utandawazi katika medani hiyo.
Masuala mengine yanayojadiliwa ni mtazamo wa Kiislamu kuhusu masuala ya watoto, jinsi ya kuwaelisha watoto na vijana wa Kiislamu kuhusu urithi wa thamani wa utamaduni wa dini yao na kuwafunza thamani za Uislamu zinazosisitiza kuwaheshimu kikamilifu na bila ya kubagua wafuasi wa dini na tamaduni mbalimbali.
Miongoni mwa shakhsia wanaohudhuria kikao hicho cha siku tatu ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la ISESCO Abdulaziz bin Othman al Tuwaijri, Katibu Mkuu wa OIC Ekmeleddin Ihsanoglu na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Amr Mussa.
Kikao cha kwanza cha Mawaziri wa Masuala ya Watoto wa nchi za Kiislamu kilifanyika tarehe 9 Novemba 2005 katika mji wa Rabat nchini Morocco. Mwishoni mwa kikao hicho kulitolewa azimio kuhusu matatizo ya watoto katika ulimwengu wa Kiislamu na njia za kukabiliana nayo. 357984

captcha