Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anaamini kwamba, hatua ya nchi za Ulaya ya kufuta jina la magaidi wa Munafiqeen wa Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi si ishara ya udhaifu wa mfumo wa Kiislamu, bali ni dalili ya nguvu ya mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imewafanya maadui wake kuchukua msimamo wa mgongano na usiokuwa wa kimantiki katika utekelezaji wa sheria za kimataifa.
Akibainisha suala hilo mbele ya waandishi habari, Ghulam Hussein Ilham, Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, kufutwa kwa kundi hilo la kigaidi katika orodha ya makundi ya kigaidi ya nchi za Ulaya si dalili ya udhaifu wa serikali wala nyombo vya kidiplomasia vya Iran, bali ni thibitisho la kutokuwa na mantiki serikali hizo za Ulaya zinazotoa madai ya uongo ya kuheshimu haki za binadamu na kutetea demokrasia duniani.
Amesema, hatua hiyo ambayo inaweka wazi madai yao yasiyo na msingi kwamba yanaheshimu haki za binadamu na kupambana na ugaidi, inapoteza imani ya taifa la Iran kwa nchi hizo na kuwa ni dalili ya wazi ya siasa zao za kundumakuwili ulimwenguni.
Msemaji huyo ambaye pia ni Waziri wa Sheria wa Iran amesema kuwa, hatua na tabia hizo za nchi za Uaya hazina thamani yoyote mbele ya taifa shupavu la Iran na kwamba kuondolewa kwa kundi hilo katika orodha ya makundi ya kigaidi hakutalisafishia jina kundi hilo ambalo linafahamika kote ulimwenguni kutokana na vitendo vyake vya ugaidi dhidi ya watu wasio na hatia nchini Iran. 360624