Shirika la habari la Bahrain (BNA) limeripoti kuwa mkutano huo unazishirikisha jumuiya zisizo za serikali kutoka nchi za Uturuki, Malaysia, Bangladesh, Misri, Kuwait, Syria na Morocco ambazo zinachunguza masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Jumuiya Zisizokuwa za Serikali katika Ulimwengu wa Kiislamu Najmi Swadiq Oglu amesema kuwa mkutano huo unajadili masuala mbalimbali kama vile ustawi endelevu, haki za binadamu, ushirikiano kati ya nchi wanachama katika kupambana na ujinga, umaskini na matatizo ya kijamii.
Swadiq Oglu amesema kuwa suala la Palestina litapewa kipaumbele katika mkutano huo hususan kwa kutilia maanani jinai na mauaji ya maelfu ya raia, uharibifu wa nyumba na idara za serikali uliofanywa na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Jumuiya Zisizokuwa za Serikali katika Ulimwengu wa Kiislamu ameongeza kuwa washiriki katika mkutano huo pia watachunguza njia za kuwasaidia wananchi wa Palestina na kwamba mkutano huo ni fursa nzuri ya kuanzisha mikakati ya kutetea haki za binadamu za raia wa Palestina.
Swadiq Oghlu amesema kuwa Palestina si suala la Waislamu pekee bali ni kadhia ya kimataifa ambayo inafuatiliwa na walimwengu wote. Amesema, makundi mbalimbali yanapaswa kushirikiana katika kutatua matatizo ya eneo hilo. 370845