Wanahistoria, wanasheria pamoja na wataalamu wa ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu wametaka uongozi wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani al-Kaaba uondolewe mikononi mwa Mawahabi na ukoo wa Saudi na kurejeshwa mikononi mwa kizazi cha Mtume Muhammad (SAW) katika Bara Arabu.
Wasomi hao na wamiliki kadhaa wa vyombo vya habari katika nchi za Kiarabu na Kiislamu wameshiriki katika kikao kilichofanyika hivi karibuni nchini Misri chini ya anwani ya 'Kizazi cha Mtume katika Bara Arabu na Kaaba Iliyozingirwa' na kusisitiza juu ya haki ya kihistoria na halali ya kizazi cha Mtume katika Bara Arabu, ya kudhibiti na kusimamia maeneo matakatifu katika bara hilo, na hasa Msikiti wa Mtume (SAW) mjini Madina na al-Kaaba mjini Makka. Washiriki wa kikao hicho vilevile wamesisitiza kwamba watafuatilia kwa karibu suala hilo katika vyombo vya sheria vya kimataifa kwa ajili ya kutoa udhibiti wa maeneo hayo kutoka mikononi mwa Mawahabi na ukoo wa Saudi na kuurejesha mikononi mwa kizazi cha Mtume (SAW). Wasomi na wanahistoria hao wamesisitiza katika utafiti wao kwamba kizazi hicho cha Mtume ndicho kilichokuwa na udhibiti wa maeneo hayo lakini utawala wa Saudi uliwaua kwa maelfu watu wa kizazi hicho mwaka 1933 na kuchukua uendeshaji wa maeneo hayo. Wamesema tokea wakati huo hadi sasa maeneo hayo matakatifu yanadhibitiwa kinyume cha sheria na utawala wa Saudia. Washiriki wa kikao hicho cha Misri pia wamezitaka taasisi za kisheria za kimataifa likiwemo Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International kusaidia kurejeshewa kizazi cha Mtume (SAW) uendeshaji na uongozi wa maeneo hayo matakatifu hasa al-Kaaba takatifu pamoja na shughuli zote za hija katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu.627966